SUDAN

Mashambulizi yaongezeka dhidi ya Jeshi la kulinda amani nchini Sudan

Vikosi vya kijeshi vya Umoja wa Mataifa vya kulinda amani nchini Sudan UNAMID vimeendelea kushambuliwa na makundi ya waasi katika jimbo la Darfur.

Matangazo ya kibiashara

Huu ni uvamizi wa tatu mwezi huu wa Agosti dhidi ya wanajeshi hao ambao siku ya Alhamisi walikuwa wanawatafuta wenzao waliopotea baada ya kutokea kwa mafuriko makubwa kutokana na mvua kubwa inayoendelea kunyesha katika jimbo hilo.

Msemaji wa idara ya habari ya UNAMID Rania Abdulrahman, amesema kuwa haijabainika wazi ni waasi gani waliovamia vikosi hivyo huku akieleza kuwa hakuna aliyejeruhiwa.

Visa vya uvamizi dhidi ya vikosi hivyo vya kulinda amani mwaka huu vimeongezeka sana  na siku ya Jumatatu wanajeshi watatu walipigwa risasi na kujeruhiwa Mashariki mwa jimbo hilo  huku wengine saba wakiuawa mwezi uliopita.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linataka oparesheni ya jeshi la UNAMID kuangaliwa upya kutokana na kudorora kwa hali ya usalama katika jimbo hilo la Darfur.

Kwa zaidi ya miaka 10 sasa waasi katika jimbo la Darfur wamekuwa wakipambana na uongozi wa serikali ya rais Omar Al Bashir kwa madai kuwa inawabagua watu weusi wanaoishi katika jimbo hilo.

Katika hatua nyingine, rais wa Marekani Barrack Obama amemteua Donald Booth kuwa mjumbe wake nchini Sudan na Sudan Kusini kujaribu kusaidia katika harakati za kuimarisha usalama na amani katika maeneo ambayo yanayokumbwa na vita.

Kabla ya kuteuliwa kwake, Booth alihudumu kama Balozi wa Marekani nchini Ethiopia na jukumu lake kubwa litakuwa ni kuhakikisha kuwa mkataba kati ya mataifa hayo mawili kuhusu usalama na biashara ya mafuta  uliokubabiliwa mwezi Septemba mwaka uliopita unatekelezwa kikamilifu.

Sudan Kusini ilijitenga na kuunda taifa lao mwaka 2011 kutoka Sudan na mataifa hayo yameendelea kuzozana kuhusu umiliki wa mipaka na maeneo yenye utajiri wa mataifa.

Serikali ya Juba na ile Khatroum zimeendelea kutuhumiana kuhusu uungwaji wa waasi katika mpaka wa mataifa hayo mawili.