RWAND-DRC

Waasi wa M 23 watangaza kusitisha makabiliano Mashariki mwa DRC

Waasi wa M 23 wanaopambana na majeshi ya serikali Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wanasema wanasitisha mapigano siku ya Ijumaa ili kuruhusu uchunguzi kufanyika kuhusu shambulizi la bomu lililorushwa nchini Rwanda na kusababisha kifo cha mwanamke mmoja na kumjeruhi mwanaye.

Matangazo ya kibiashara

Kiongozi wa kundi hilo Betrand Bissimwa ameimbia RFI kuwa wanajeshi wake wanaondoka katika eneo la Kanyaruchinya ili kuruhusu kufanyika kwa uchunguzi huo kubaini ni nani hasa aliyerusha kombora  hilo.

Bissimwa amekanusha kuwa wanasitisha mapigano baada ya jeshi la serikali kudai kuwa limewadhoofisha na kuongeza kuwa vikosi vyake vitaendelea kupiga kambi katika ngome wanazothibiti na bado wako imara.

Serikali ya Rwanda inalituhumu jeshi la serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kurusha makombora  katika wilaya ya Rubavu siku ya Alhamisi.

Madai ya Rwanda yanakanushwa na jeshi la DRC ambalo linalituhumu kundi la waasi wa M 23 kurusha mabomu hayo wakati huu mapambano yakiendelea Mashariki mwa nchi hiyo.

Wanajeshi la Umoja wa Mataifa wanasema kuwa waliwaona waasi wa M 23 wakirusha makombora hayo nchini Rwanda wakati wakiwa katika viwanja vya mapambano.

Kigali inasema kuwa jeshi la Kinsasha lilirusha mabomu 10 katika mji wa Gisenyi siku ya Alhamisi asubuhi na kuwalenga raia wake waliokuwa sokoni na wale wanaoishi karibu na DRC.

Waziri wa Mambo ya nje wa Rwanda Louise Mushikiwabo amesema mashambulizi katika mipaka ya nchi yake hayakubaliki kamwe na ni lazima yakomeshwe huku akieleza kuwa kwa kipindi cha mwezi mmoja uliopita, zaidi ya mabomu 30 yamerushwa nchini Rwanda na jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Tuhma hizi kati ya Kigali na Kinsasha zinakuja siku moja baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kusema kuwa ina ripoti za kuaminika kuwa serikali ya Rwanda inawaunga mkono waasi wa M 23 wanaopambana na wanajeshi wa DRC.

Rwanda imeendelea kupinga madai ya Umoja wa Mataifa kuwa inawafadhili na kuwaunga mkono waasi hao wa M 23 ambao mwaka uliopita waliuteka mji wa Goma kwa siku 10.

Mapigano yanaendelea kwa wiki moja sasa kati ya waasi hao na jeshi la DRC likisadiwa na vikosi vya Umoja wa Mataifa karibu na mji wa Goma na mapema juma hili mwanajeshi wa kulinda amani kutoka nchini Tanzania aliuawa katika mapambano hayo.

Mazungumzo ya amani kati ya serikali ya Kinsasha na waasi wa M 23 yamegonga mwamba jijini Kampala Uganda suala ambalo limeendelea kuhatarisha usalama Mashariki mwa nchi hiyo.

Mzozo wa Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo umekuwa ukiendelea kwa kipindi kirefu na ulizorota mwaka uliopita baada ya kuzuka kwa kundi la M23 lililodai kubaguliwa na serikali ya Kinsasha.