MISRI

Wafuasi wa Morsi waapa kuendelea kuandamana nchini Misri

Wafuasi wa rais wa zamani wa Misri aliyeondolewa madarakani Mohamed Morsi wanasema kuwa wataendelea na maandamano kila Ijumaa licha ya kukamatwa kwa viongozi wao katika oparesheni inayoendelea nchini humo.

Matangazo ya kibiashara

Wito wa kufanyika kwa maandamano haya unakuja baada ya serikali ya mpito kutangaza kuwa imemkamata mwanasiasa wa kundi la Muslim Brotherhood, Mohamed al-Beltagi karibu na mji wa Cairo.

Polisi pia wanasema kuwa wamefanikiwa kuwakamata wafuasi wengine 28 wa Muslim Brotherhood jijini Cairo katika oparesheni ambayo pia imeanza kutekelezwa katika sehemu zingine nchini humo.

Wizara ya Mambo ya ndani inasema kuwa polisi watatumia silaha za moto ikiwa waandamaji watavamia majengo ya serikali na kuhatarisha usalama wa raia wengine wakati wa maandmano yao .

Tangu kuondolewa jijini Cairo, wafuasi wa Morsi wamekuwa wakiandamana kila siku kuendelea kushinikiza kuachiliwa huru na kurejeshwa madarakani kwa kiongozi wao Mohammed Morsi wanayesema alichaguliwa kidemokrasia.

Zaidi ya watu 1,000 waliuawa mwezi uliopita wakati jeshi na polisi liliposhirikiana kuwaondoa wafuasi wa Mosri jijini Cairo na kuwakamata wengine zaidi ya 2,000 wanaozuliwa katika jela mbalimbali nchini humo.

Viongozi wa Muslim Brotherhodd wamekuwa wakituhumiwa na serikali ya mpito kwa kusababisha machafuko nchini humo na kuwashawishi wananchi wake kuendelea kupiga kambi jijini Cairo.

Juhudi za Marekani kujaribu kutatua mzozo wa kisiasa nchini humo ziliambulia patupu huku rais wa zamani Mohammed Morsi akiendelea kuzuiliwa na jeshi.

Mamilioni ya wananchi wa Misri walimwondoa Mosri uongozini baada ya kumtuhumu kushindwa kuimarisha maendeleo ya haraka ya kiuchumi na pia kwa kumshtumu kujilimbikizia madaraka.