MALI

Dioncunda Traore ajivunia mafanikio yaliyofikiwa nchini Mali

RFI

Serikali ya Mali imefanikiwa kukabiliana na Changamoto iliyokuwa ikiwakabili ya kurejesha hali ya usalama nchini humo baada ya kuingia katika mgogoro wa kisiasa, Kiongozi wa mpito Dioncunda Traore,ambaye anamaliza muda wake juma hili ameeleza.

Matangazo ya kibiashara

Akiongea katika mkutano wake wa mwisho na mawaziri wa nchini humo,kabla ya Rais mteule Ibrahim Boubakar Keita kuapishwa siku ya jumatano, Traore amepongeza Serikali yake ambayo amesema imefanikiwa kutekeleza jukumu gumu lililokuwa mbele yao.

Baada ya kuingia madarakani mwezi Aprili mwaka Jana, Traore na Serikali yake walikuwa na jukumu la kurejesha hali ya usalama na kuandaa uchaguzi ulio huru na haki.

Uchaguzi uliompa ushindi Keita tarehe 11 mwezi Agosti umefungua milango kwa ufaransa kupunguza jeshi lake lililokuwa likisaidia serikali ya mali kupambana na Wanamgambo kaskazini Mwa nchi hiyo.

Amesema kuwa Mali imekuwa ikirejea polepole katika hali yake ya klawaida baada kukaibiliwa na uasi na ugaidi uliokuwa ukifanywa na waasi wa Tuareg na waislam wenye msimamo mkali wanaohusishwa na kundi la kigaidi la Al Qaeda.

Traore alisema kuwa amefurahishwa sana na uungwaji mkono wa Jumuiya ya Kimataifa amba umeisaidia Mali kurejea hali ya kawaida baada ya kupitia misukosuko mikubwa.