ZIMBABWE

Shirika la Kimataifa la Kutetea Haki za Binadamu lamtaka Rais Robert Mugabe aheshimu haki za binadamu

Shirika la Kimataifa la Kutetea Haki za Binadamu, Human Rights Watch, HRW limemtaka Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe kutoa kipaumbele kwenye harakati za kulinda haki za binadamu baada ya kuchaguliwa tena katika uchaguzi ambao HRW wanaona uligubikwa na hila.

REUTERS/Philimon Bulawayo (
Matangazo ya kibiashara

Mkurugenzi wa HRW wa kanda ya Kusini mwa Afrika Tiseke Kasambala amesema kuwa Rais Mugabe anawajibika kuiweka Zimbabwe katika mkondo unaoheshimu utawala wa kidemokrasia.

Kasambala amesema Mugabe akiweka kipaumbele katika ajenda ya kulinda haki za binadamu basi rais huyo atakua anatuma ujumbe kwa dunia kuwa Zimbabwe inaimarika kidemokrasia.

Ameutaka utawala mpya wa Mugabe kuweka mikakati mipya kwa kuweka muundo mpya wa kiutawala unaoheshimu haki za binadamu ili kuondokana na rekodi mbaya ukiukwaji wa haki z binadamu ambayo Zimbabwe imekuwa nayo.

HRW imependekeza kuwa ili Zimbabwe ifanikiwe katika hilo lazima ikomeshe ukiukwaji wa haki za binadamu, iweke mazingira ya uwepo wa uhuru wa vyombo vya habari na uhuru kwa wanaharakati kuandaa mikutano na maandamano kulingana mahitaji.

Shirika hilo lisema ni vema kukachukuliwa hatua za haraka kuanzisha tume ya haki za bindamu yenye viwango vya kimataifa ili kuonyesha ulimwengu kuwa Zimbabwe inaheshimu haki za binadamu.

Mugabe alishinda tena urais katika uchaguzi uliofanyika Julai 31 mwaka 2013 huku akijinyakulia asilimia 61 za kura zilizopigwa wakati chama kikuu cha upinzani cha Movement for Democratic Change uliambulia asilimia 34.