AFRIKA KUSINI

Wamiliki wa migodi Afrika Kusini watoa mapendekezo mapya ya nyongeza ya mshahara wafanyakazi

Wamiliki wa migodi nchini Afrika Kusini hii leo wametoa mapendekezo mapya ya nyongeza ya mshahara kwa maelfu ya wafanyakazi wa mgodini waliogoma kwa lengo la kujaribu kusitisha mgomo ambao umeingia siku yake ya tatu hii leo.Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na chama cha kitaifa cha kutetea maslahi ya wafanyakazi wa mgodini NUM, imesema kuwa viongozi wake wanaendelea kujadili mapendekezo yaliyowasilishwa na wamiliki wa migodi na kisha watayatolea uamuzi.

RFI
Matangazo ya kibiashara

Msemaji wa NUM, Lesiba Seshoka amethibitisha kupokea ofa toka kwa wamiliki hao na kuongeza kuwa haimaanishi kuwa wanasitisha mgomo wao wala haimaanishi kuwa ofa hiii mpya itatoa hakikisho la wao kurejea kazini na kwamba wanaendelea kuijadili.

Awali makampuni hayo yalipendekeza nyongeza ya asilimia 6.5 kiwango ambacho wafanyakazi hao wanadai hakitoshi na wanataka kifikie asilimia 10 ambayo ni sawa na asilimia 60 ya mshahara halisi.

Chama cha NUM ambacho kinawanachama zaidi la elfu sabini nchini nzima kimeendelea kutafuta uungaji mkono toka kwa wafanyakazi wengine ambao wamejitenga na kuunda chama cha wafanyakazi wa ujenzi na migodini AMCU ambacho kinadai NUM ni tawi la chama tawala cha ANC.

Sekta ya madini inapoteza kiasi cha dola milioni 34 kila siku kutokana na migomo hii.