Zimbabwe-Rushwa

Polisi nchini Zimbabwe yatangaza kuanzisha uchunguzi dhidhi ya mtu wa karibu na rais Mugabe

Polisi nchini Zimbabwe hii leo wametangaza kuanzisha uchunguzi rasmi dhidi ya tuhuma za rushwa zinazomkabili afisa mmoja wa karibu wa rais Mugabe anayedaiwa kutaka kupokea rushwa ya dola milioni 6 toka kwa mwekezaji kutoka nchini Ghana aliyetaka kuwekeza kwenye sketa ya madini.

Polisi nchini Zimbabwe
Polisi nchini Zimbabwe
Matangazo ya kibiashara

Msemaji wa polisi nchini humo, Charity Charamba amesema kuwa tuhuma dhidi ya aliyekuwa mwenyekiti wa kamati ya madini, Godwills Masimirembwa zinahitaji uchunguzi na ndio maana baada ya kuibuliwa bungeni wameamua kuanzisha uchunguzi dhidi yake.

Masimirembwa anadaiwa baada ya kuingia mkataba na kampuni moja ya uchimbaji madini ya nchini Ghana anadaiwa kutaka kiasi cha dola za Marekani milioni 6 ili kuruhusu kampuni hiyo kuingiza vifaa vyake nchini humo akidai walikiuka masharti ya mkataba.

Juma moja lililopita rais Robert Mugabe aliapa kupambana na viongozi wala rushwa na kuagiza kufanyika uchunguzi kuhusu tuhuma za maofisa wa serikali yake.

Katika hatuwa ambayo sio ya kawaida ya kinidhamu, Chama cha rais Mugabe, kimewasimamisha uanachama viongozi watano wa ngazi za juu wa chama hicho kutoka na tuhuma zinazo wakabili za kuhusika na rushwa katika makampuni ya uchimbaji madini ya kigeni.