GUINEA

Mapigano mapya yazuka nchini Guinea ikiwa ni siku chache zimesalia kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu

Reuters

Mapigano ya meshuhudiwa katika siku ya tatu mfululizo kwenye mji wa Conakry nchini Guinea wakati huu Taifa hilo likijiandaa kufanya uchaguzi wake mkuu tarehe 28 ya mwezi huu. Usiku wa kuamkia leo jumatano kumeshuhudiwa machafuko kwenye mji wa Ratoma ambapo maduka kadhaa yamechomwa.

Matangazo ya kibiashara

Waziri wa haki za binadamu na uhuru wa umma wa nchini humo Kalifa Gassam Diaby ametoa wito kwa wananchi kuwa watulivu ili kuruhusu zoezi la uchaguzi kukamilika kama ilivyopangwa.

Kwenye vurugu za siku ya jumatatu polisi mmoja aliuawa huku watu zaidi ya 70 wakijeruhiwa kwenye makabiliano ya wafuasi wa chama tawala na wale wa upinzani mjini Conakry.

Serikali imeendelea kutoa wito kwa vyama vya kisiasa kuwahimiza wanachama wao wapunguze hasira ili kuepusha madhara zaidi yanayoendelea kuligawa Taifa hilo.

Kiongozi mkuu wa upinzani katika Taifa hilo Cellou Delein Diallo amekuwa akiushutumu upande wa Rais Conde kuwa katika mchakato wa kutumia mbinu chafu ili kupotosha ukweli wa matokeo halisi ya kura zitakazopigwa katika uchaguzi huo.

Bado maandalizi ya zoezi hilo yameonekana kusasua na mpaka sasa inaelezwa kuwa bado tume ya uchaguzi haijaweka wazi orodha kamili ya wananchi watakaopiga kura.

Kura za wabunge zilipaswa kupigwa miezi sita baada ya Rais wa nchi hiyo Alpha Conde kuapishwa mwezi Desemba mwaka 2010 lakini zoezi hilo limekuwa likikwama kutokana na migongano ya mara kwa mara.