SUDAN

Vurugu zaidi zaendelea kushuhudiwa nchini Sudani huku vikosi vya usalama vikidaiwa kuua watu wapatao 50

Vurugu zimeendelea kushuhudiwa nchini Sudani hii leo siku ya tano tangu wananchi waanze maandamano kupinga uamuzi wa serikali kuongeza tozo katika bei za mafuta, ambapo polisi wanadaiwa kuwaua waandamanaji wapatao hamsini kwa kuwapiga risasi. 

Vurugu za waandamanaji wakichoma vituo vya mafuta nchini Sudani
Vurugu za waandamanaji wakichoma vituo vya mafuta nchini Sudani tucumcari.plateautel.net
Matangazo ya kibiashara

Wanaharakati wametoa wito kwa waandamanaji kuandamana mitaani baada ya sala ya Ijumaa kila wiki, na vikosi vya usalama vimesambazwa karibu na majengo ya serikali, ikiwa ni pamoja na askari kadhaa.

Wanajeshi wameonekana wakilinda kituo cha mafuta ya Petroli mjini Khartoum kilichofunguliwa kwa ajili ya biashara, huku mistari mirefu ya magari ikisubiri kujaza mafuta.

Akiungana na wanaharakati vijana, Waziri mkuu wa zamani na kiongozi wa chama kikuu cha upinzani cha Al-Umma Sadeq al-Mahdi ametoa wito kwa raia wa Sudani kuendeleza maandamano.

Aidha mamlaka nchini humo imezuia usambazwaji wa nakala za magazeti matatu kwa lengo la kujaribu kukomesha kuenea kwa machafuko inagwa magazeti hayo yanadaiwa kuunga mkono serikali.

Maandamano haya yanatajwa kuwa makubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa nchini humo tangu rais Bashir aingie madarakani mwaka 1989.