KENYA-ICC

Shahidi wa pili katika ya kesi ya Ruto na Sang aanza kutoa ushahidi wake ICC

Shahidi wa pili katika kesi inayomkabili naibu rais wa Kenya William Ruto na Mtangazaji Joshua Arap Sang katika Mahakama ya Kimataifa ya ICC mjini Hague wakotuhumiwa kufadhili na kuchochea machafuko ya baada ya uchaguzi Mkuu mwaka 2007 ameanza kutoa ushahidi wake mbele ya Majaji wa Mahakama hiyo. 

Matangazo ya kibiashara

Jaji kiongozi katika kesi hiyo Chile Eboi-Osuji aliamuru kuwa shahidi huyo anayefahamika kwa namba 326 atatoa ushahidi wake wazi ili umma upate nafasi ya kufuatilia ushahidi wake.

Hata hivyo, jina la shahidi huyo halikutajwa, wala sura yake kuonekana na sauti yake ilibadilishwa ili kumlinda kwa mujibu wa sheria za kuwalinda mashahidi.

Shahadi huyo alianza kwa kueleza namna chama cha ODM kilivyohusika na machafuko katika eneo la Rift Valley mwaka 2007 chini ya Ruto ambaye kipindi hicho alikuwa mmoja wa kigogo wa chama hicho.

Aidha, shahidi huyo amedai kuwa ana ushahidi kuwa chama cha ODM kilimpa Ruto kiasi kikubwa cha fedha kuwalipa vijana ili wazue fujo katika eneo hilo la Rift Valley.

Ni siku ya kwanza ya kutoa ushahidi wake mbele ya Mahakama hiyo, shahidi huyo ametumia muda mwingi akielezea muundo wa chama cha ODM wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2007 chini ya Raila Odinga ambaye wakati huo alikuwa mgombea urais.

Tayari shahidi wa kwanza ametoa ushahidi wake ambao aliutoa kwa siri baada ya jina lake kuanza kusambazwa katika mitandao ya kijamii na kuhatarisha maisha yake suala ambalo lilisababisha Majaji wa Mahakama hiyo kuamuru kuwa ushahidi wake utolewe kwa siri.

Mbali na kesi inayomkabili naibu rais Ruto na Mtangazaji Joshua Sang, rais Uhuru Kenyatta pia anakabiliwa na kesi ya kujibu katika Mahakama hiyo na kesi yake inatarajiwa kuanza mwezi Novemba.

Uhuru atakuwa rais wa kwanza duniani akiwa uongozini kushtakiwa katika Mahakama hiyo kutokana na tuhma za kuhusika na visa vya ukiukwaji wa haki za binadanu vilivyotokea nchini Kenya na kusababisha zaidi ya watu elfu moja kupoteza maisha na maelfu kukimbia makwao.