AU-ICC

Umoja wa Afrika wasema Mahakama ya Kimataifa ya ICC inawaonea Waafrika

Mawaziri wa Mambo ya nje wa nchi za Afrika wameyashtumu Mahakama ya Kimaifa ya ICC kwa kutowatendea haki na kuwaonea Waafrika.

Matangazo ya kibiashara

Shutuma hizo zimetolewa katika  siku ya kwanza ya kikao kisicho cha kawaida cha viongozi hao jijini Addis Ababa Ethiopia kabla ya kuhudhuriwa na marais siku ya Jumamosi.

Waziri wa Mambo ya nje wa Ethiopia Tedros Adhanom Ghebreyesus amewaambia Mawaziri wenzake kuwa Mahakama hiyo inawalenga tu Waafrika na haki haiwezi kupatikana katika Mahakama hiyo.

Awali Umoja wa Afrika uliomba kesi inayowakabili viongozi wa Kenya kurudishwa nyumbani kwa madai kuwa kuwepo kwao Hague kungehitilafiana na uongozi wao kama viongozi wa Kenya.

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ameiomba Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita ya ICC kusitisha kesi ya uchochezi, ufadhili na kupanga machafuko ya baada ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2007 inayomkabili.

Kupitia kwa Mawakili wake, Kenyatta anasema anaamini kuwa haki haitapatikana katika Mahakama hiyo kwa sababu Mashahidi dhidi yake wameshirikiana na upande wa Mashtaka kutoa ushahidi wa uongo.

Aidha, Kenyatta anasema kuwa mashahidi wake wametishwa na upande wa Mashtaka na kulazimishwa kubadilisha ushahidi wao.

Ombi hili la rais Kenyatta linakuja siku mbili tu baada ya Waziri wa Mambo ya nje wa nchi hiyo Amina Mohammed kusema kuwa hakuna rais yeyote duniani ambaye amewahi kushtakiwa katika Mahakama hiyo au Mahakama nchini mwake akiwa uongozini.

Wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu nchini Kenya mapema mwaka huu rais Kenyatta aliahidi kushirikiana na Mahakama hiyo hata kama angechaguliwa kuwa rais na kusema kuwa kesi inayomkabili ilikuwa ya kibinafsi.

Bunge la Kenya mwezi uliopita lilipitisha mswada wa Kenya kujiondoa katika mkataba wa Roma unaotambua Mahakama hiyo na kutoa wito kwa mataifa mengine kufuata mfano huo.

Naibu rais William Ruto ambaye kesi yake inaendelea katika Mahakama hiyo anarejea nchini Kenya Ijumaa usiku ili kumruhusu rais Kenyatta kuhudhuria kikao hicho cha Umoja wa Afrika .

Katiba ya Kenya hairuhusu rais na naibu wake kuwa nje ya nchi hiyo kwa wakati mmoja.

Ruto anatarajiwa kurejea mjini Hague siku ya Jumapili.