KENYA-ICC

Bensouda awataka Majaji wa ICC kubadilisha uamuzi wa kumruhusu rais Kenyatta kutohudhuria vikao vyote

Kiongozi wa Mashtaka katika Mahakama ya Kimataifa ya ICC Fatoue Bensouda ametoa ombi kwa Majaji wa Mahakama hiyo kubadilisha uamuzi wao wa hapo awali kumruhusu rais wa Kenya Uhuru Kenyatta kutohudhuria vikao vyote wakati kesi yake itakapoanza mwezi ujao.

Matangazo ya kibiashara

Bensouda amesema kuwa washtakiwa wote wanastahili kupewa haki sawa mbele ya Mahakama hiyo na hivyo ni muhimu kwa Majaji kubadilisha uamuzi wao ili rais Kenyatta ahudhurie vikao vyote.

Ombi la Bensouda linakuja baada ya Majaji wa Mahakama hiyo wiki iliyopita kuamua kuwa Naibu Rais William Ruto atahitajika kuhudhuria vikao vyote vya kesi yake inayoendelea baada ya ombi lake la kutaka kutohudhuriwa vikao vyote kukataliwa na Mahakama hiyo.

Ijumaa iliyopita, Mahakama hiyo ilimpa nafasi Ruto kurudi nyumbani ili kumruhusu rais Kenyatta kuzuru nchi ya Rwanda katika ziara ya siku mbili ya kikazi na anatarajiwa kurudi Hague siku ya Jumatano.

Shahidi wa sita katika kesi inayomkabili Ruto na Mtangazaji Joshua Arap tayari amaeanza  kutoa ushihidi wake mbele ya Mahakama hiyo kuelezea namna wawili hao walivyoshirikiana kupanga na kufadhili machafuko ya baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2007.

Nchini Kenya waandani wa rais Kenyatta wameendelea kumshawishi kutohudhuria vikao hivyo vya ICC baada ya Umoja wa Afrika kupitisha azimio mapema mwezi huu kutaka Mahakama hiyo ya Kimataifa kuahirisha kesi inayowakabili viongozi wa Kenya ili kuwaruhusu kutekeleza majukumu yao ya Kikatiba.

Nao muungano wa upinzani nchini humo CORD unakutana jijini Nairobi chini ya uongozi wa aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga kutafuta msimamo wa pamoja kuhusu shinikizo za serikali kutaka kesi inayowakabili viongozi wa Kenya kuahirishwa.