SUDAN-SUDAN KUSINI-ABYEI

Wakaazi wa Abyei wasubiri matokeo ya kura ya maoni

Wakaazi wa jimbo la Abyei nchini Sudan waliopiga kura ya maoni kwa siku tatu zilizopita kuamua wanataka eneo hilo kuwa nchi ya Sudan au Sudan Kusini wanasubiri matokeo ya kura hiyo.

Matangazo ya kibiashara

Waandalizi wa zoezi hilo lililoandaliwa na watu wa Kabila la Dinka Ngok wamekashifiwa na Umoja wa Afrika kwa kile inachosema ni hatari kwa usalama wa nchi ya Sudan na Sudan Kusini.

Nchi za Sudan na Sudan Kusini hazitambui kura hiyo ya maoni baada ya viongozi wa nchi hizo mbili zinazowania eneo hilo lenye utajiri wa mafuta kushindwa kuafikana tarehe ya upigaji kura na ni nani wanaostahili kushiriki katika zoezi hilo.

Viongozi wa Kabila la Dinka -Ngok wanasema kuwa waliamua kuendelea na zoezi hilo baada ya kusubiri kwa muda mrefu kupatikana kwa muafaka kati ya serikali ya Khartoum na Juba kuhusu kura hiyo ya maoni bila mafanikio.

Wilson Rodiong kiongozi wa upinzani nchini Sudan Kusini ambaye pia ni mmoja wa Waandalizi wa kura hiyo amesema kuwa wameshangazwa na ukosoaji wa Umoja wa Afrika kwa kile ambacho anasema ni wao ndio waliokuwa wamepanga kufanyika kwa kura hiyo ya maoni kufikia mwisho wa mwezi wa Oktoba.

Katika hatua nyingine, kiongozi wa Kabila lenye asili ya Kiarabu la Misseriya ambalo linasema ni sharti lishirikishwe katika upigaji kura huo linaonya kuwa litaishambulia kabila la Dinka-Ngok ikiwa litatangaza kuwa jimbo hilo liko Sudan Kusini.

Kiongozi wa Kabila hilo Mohammad Omar Al Ansary akizungumza jijini Khartoum siku ya Jumanne alisema kuwa Kabila la Dinka Ngok limechukua sheria mikononi mwao na walichofanya sio sahihi.

Mapema juma hili, rais wa Sudan Omar Al Bashir alisema kuwa atahakikisha kuwa anapata ufumbuzi wa eneo la Abyei baada ya kuzuru Sudan Kusini wiki iliyopita na kushindwa kuafikiana na mweyeji wake Salva Kiir ni lini kura hiyo ya maoni ingefanyika.

Watu wa Abyei walistahili kupiga wanataka kuwa raia wa nchi gani wakati wenzao wa Sudan Kusini walipokuwa wanapiga kura ya kujitenga na Sudan mwaka 2011 lakini mzozo umesalia kuhusu ikiwa kabila la kuhamahama la Misseriya lishiriki katika zoezi hilo au la.