NIGERIA-BOKO HARAM

Pendekezo la kuongezwa muda wa hatari nchini Nigeria laidhinishwa rasmi na bunge

Reuters

Bunge la seneti nchini Nigeria limepitisha pendekezo la Rais Goodluck Jonathan lililotaka kuongezwa muda wa hali ya hatari kwa kipindi cha muda wa miezi sita zaidi katika baadhi ya maeneo yanayokabiliwa na hofu ya usalama. Maseneta wamepigia kura na kuunga mkono pendekezo hilo linalogusa majimbo ya Adamawa, Borno na Yobe.

Matangazo ya kibiashara

Mwezi Mei Rais Jonathan alilazimika kutangaza hali ya hatari katika majimbo hayo matatu kutokana na kuendelea kutekelezwa kwa mauaji yanayoendeshwa na kundi la kiislamu la Boko Haram.

Barua ya Rais Jonathan iliyowasilishwa kwa wabunge siku ya jumatano, ilibainisha kuwa jeshi lake limefanikiwa kukabiliana na wanamgambo hao lakini bado kuna changamoto kadhaa za kiusalama ambazo zinapaswa kushughulikiwa katika muda wa tahadhari ulioongezwa.

Jeshi la Nigeria limekuwa katika operesheni kwa lengo la kulitokomeza kundi hilo lililoanza harakati zake mwaka 2009 lakini bado haijawezekana kusambaratisha ngome za wanamgambo hao.

Boko Haram wamekuwa wakiendesha mashambulizi kutaka serikali ya Nigeria itambue utawala wa sheria ya kiislamu na kupingana na mwenendo wa sasa wanaodai umegubikwa na itikadi za Mataifa ya magharibi.