COTE D'IVOIRE

Serikali ya Cote d'Ivoire inapania kuwaachia huru kwa muda wafungwa ili kupunguza msongamano katika jela.

Rais wa Cote d'Ivoire, Alassane Ouattara amefahamisha leo jumatatu kwamba serikali yake inapania kuchukua hatua mpya ili kupunguza msongamano wa wafungwa katika jela mbalimbali nchini humo. Hatua hio inahusu tu wafungwa waliyokua mbaroni kufuatia machafuko yaliyotokea baada ya uchaguzi, ili kuboresha maridhiano na kudumisha amani, amesema Alassane Ouattara.“ Nimemuomba waziri wa sheria kutathmini upya hatua zingine zitakazo ambatana na kupunguza msongamano wa wafungwa katika jela, katika hali ya kuboresha maridhiano na kudumisha amani nchini mwetu, amesema Alassane Ouattara, akijibu kuhusu mapendekezo ya mabalozi wa nchi za kigeni nchini Cote d'Ivoire.

Matangazo ya kibiashara

Katika hotuba yake ya mwisho wa mwaka, Ouattara alifahamisha kwamba baadhi ya wafungwa kufuatia machafuko yaliyotokea baada ya uchaguzi wataachiwa huru kwa muda.

Mabalozi nchini Cote d'Ivoire wamekua wakipendekeza baadhi ya wafungwa waliyoziwiliwa kutokana na machafuko yaliyotokea baada ya uchaguzi waachiwe huru kwa muda, na kupongeza jitihada zinazofanywa kwa kuboresha maridhiano hadi mwaka 2014.

“Mabalozi wa nchi za kigeni hapanchini Cote d'Ivoire, wanakupongeza kwa kuendelea na jitihada za kuboresha maridhiano hadi mwaka 2014”, amesema Askofu Joseph Stiter, balozi wa Vatican nchini Cote d'Ivoire, ambae anaongoza kundi la mabalozi wa kigeni nchini Cote d'Ivoire.

Askofu Stiteri ameomba pia mazungumzo na vyama vya upinzani yaweze kuendelea.
Mwanzoni mwa mwezi wa nane, vyombo vya sheria vilimuachia huru raia wa ufaransa mwenye asili ya Cote d'Ivoire, mwanae Laurent Gbagbo, Michel Gbagbo, Pascal Affi N'Guessan, aliekua kiongozi wa chama tawala cha zamani cha (FPI), na Justin Koua, kiongozi wa kundi la vijana kutoka chama cha (FPI), na wengineo.

Mamia ya wafuasi wa Laurent Gbagbo wanaziwiliwa kufuatia machafuko yaliyotokea baada ya uchaguzi.

Zaidi ya watu 3000 walipoteza maisha kati ya mwaka 2010 hadi mwezi aprili mwaka2011, baada ya Gbagbo kukataa kutambua ushindi wa mpinzani wake Alassane Ouattara katika uchaguzi wa urais uliyofanyika mwezi wa novemba mwaka 2010.

Laurent Gbagbo anaziwiliwa mjini La Haye kwa kusubiri kesi inayomkabili ya uhalifu dhidi ya binadamu.