NIGERIA-Usalama

Nigeria yaendelea kukumbwa na visa vya mauwaji

RFI

Polisi nchini Nigeria wanasema watu zaidi ya 17 wamepoteza maisha katika katika kijiji kimoja cha jimbo la Plateau baada ya kuvamiwa na watu waliojihami kwa silaha mwanzoni mwa juma hili. Gavana wa jimbo hilo Chris Olakpe amesema kati ya watu hao watano waliteketea kwa moto na nyumba zaidi ya 20 kuchomwa moto.

Matangazo ya kibiashara

Wenyeji wanasema tofauti kati ya makabila ya Husana na Fulani ndio chanzo cha uvamizi huo, na kusababisha idadi kubwa ya vifo katika siku za hivi karibu katika taifa hilo ambalo linashuhudia ukosefu wa usalama, Kaskazini mwa nchi hiyo.

Katika kijiji hicho kinachopatikana eneo la kati mwa Nigeria kunaishi watu wa dini mbali mbali.

Kijiji hicho kiko katika eneo ambalo limekuwa likikumbwa na mzozo wa muda mrefu wa kikabila.

Watu waliokuwa wamejihami walishambulia kijiji cha Shonong nyakati za asubuhi juzi jumatatu, huku wakiwapiga risasi wenyeji na hata kuteketeza nyumba zao.

Washambuliaji wanaoaaminika kutoka jamii ya Fulani pia waliiba mifugo.

Msemaji wa kijeshi katika eneo hilo alithibitisha mauaji hayo lakini akasema kuwa ni mapema mno kuelezea idadi kamili ya watu waliouawa, ingawa uchunguzi zaidi unaendelea kufanywa.

Maelfu ya watu wameuawa katika kipindi cha miaka mitatu katika mashambulizi ya kulipiza kisasi kati ya makabila hasimu katika mkoa wa kusini wenye wakristo na kaskazini wanakoishi waislamu.

Vurugu katika eneo la Kati mwa Nigeria huchochewa na mizozo ya ardhi kati ya wahamiaji kutoka jamii ya Fulani na wakulima kutoka jamii ya Berom ambao ni wakristo.

Hayo yanajiri wakati, mwaka 2010 maafu ya watu wameuawa katika mizozo kama hiyo, wakiwemo watoto na wanawake.