RWANDA-Justice

Familia ya aliekua rais wa Rwanda Juvenal Habyarimana inaomba kufanyike uchunguzi kuhusu kifo cha kiongozi huyo

RFI

Familia ya rais wa zamani wa Rwanda Juvenal Habyarimana, inataka Uchunguzi ufanyike ili kubaini nani alihusika katika udunguaji wa ndege iliokuwa ikiwasafirisha marais wa Rwanda Juvenal Habyarimana na Cyprien Ntaryamira wa Burundi, ikiwa ni miaka ishirini sasa baada ya tukio hilo, la mwaka 1994 uchunguzi kuhusu shambulio hilo bado unaonekana kugonga mwamba. 

Matangazo ya kibiashara

Mwezi Julai mwaka uliopita, aliyekuwa mkuu wa Intelijensia nchini Rwanda hayati Patrick Karegeya alitangaza dhahiri shahiri kwamba alikuwa na ushahidi wa kuhusika kwa Rais wa Rwanda Paul Kagame katika shambulio hilo, sambamba na Jeneral Kayumba Nyamwasa alieyekimbilia uhamisho nchini Afrika Kusini.

Mwendesha Mashtaka nchini Ufaransa Marc Trevidic ameomba mara kadhaa Kayumba Nyamwasa asafirishwe hadi nchini humo kutoa ushahidi wake, jambo ambalo hadi sasa halijafanikiwa.

Marais Juvenal Habyarimana na Cyprien Ntaryamira waliuawa wakitokea nchini Tanzania katika mchakato wa kusaka amani nchini Rwanda, baada ya waasi wa kundi la RPF wakati huo, ambalo kwa sasa ni chama madarakani, kuanzisha vita vya maguguni dhidi ya serikali ya Juvenal Habyarimana, wakimtuhumu kuwatenga raia wa Rwanda kutoka jamii ya watutsi.

Ndege waliyokuwemo marais hao wawili ilidunguliwa kwa kupigwa roketi ilipokua ikijaribu kutua kwenye uwanja wa Kanombe, mjini Kigali.

Kifo cha Juvenali Habyarimana kilipelekea wafuasi wake (Interahamwe) kutoka chama cha MRND, kilichokua chama tawala wakati huo, na washirika wao kupandwa na hasira na kuanza kujilipiza kisase wakiwalenga raia kutoka jamii ya watutsi na wahutu wenye msimamo wa wastani.

Watu 800,000 kutoka jamii ya watutsi na wahutu wenye msimamo wa wastani, ambao walikua hawaungi mkoano harakati za chama cha MRND, wanarifiwa walipoteza maisha katika machafuko hayo.