RWANDA-Siasa

Chama cha aliekua waziri mkuu wa Rwanda chaungana na kundi la wanamgambo wa kihutu la FDLR

RFI

Waziri Mkuu wa zamani nchini Rwanda Faustin Twagiramungu aishiye uhamishoni amesema chama chake cha Rwanda Dream Initiative kimeungana na waasi wa Kihutu wa FDLR walioko nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Twagiramungu ameshirikiana pia na chama cha PS Imberakuri cha Bwana Bernard Ntaganda aliye kifungoni kwa tuhuma za kujenga chuki na utengano nchini rwanda.

Matangazo ya kibiashara

Lengo la muungano huo kwa mujibu wa Twagiramungu ni kuruhusu wakimbizi wote wa Rwanda kurudi nyumbani pamoja na vyama vingine vya upinzani viliyoko uhamishoni ili kuiomba Jumuiya ya kimataifa ishinikize serikali ya rais Paul Kagame kuandaa mazungumzo ya kitaifa na wapinzani wake.

“Sasa ni wakati wa kukomesha propaganda ya Kigali hususan ya Kagame, ambae anatumia mauwaji ya kimbari kwa kumnyooshea kila mtu eti amefanya mauwaji hayo.

Nafikiri kuwa wanyarwanda waliokimbia tangu mwaka 1996 na waishio kwenye misitu ya Congo hawakutekeleza mauwaji hayo. Katika Muungano huu, tunataka Jumuiya ya Kimataifa itusaidie tuanze mazungumzo na serikali ya Kigali, hatuwezi kuendelea hivi, nadhani ikiwa kuna wahalifu ndani ya misitu ya Kongo, wapo pia waalifu nchini Rwanda” amesema Twagiramungu.

Hayo yakijiri, msemaji wa polisi nchini Msumbuji Joao Machava ameekanusha jana taarifa za polisi kuwatia nguvuni raia 4 wa Rwanda wanaoshukiwa kutekeleza mauaji ya aliyekuwa kiongozi wa idara ya ujasusi nchini Rwanda Patrick Karegeya aliyeuawa mwanzoni mwa mwaka huu.

Taarifa hii ya jeshi la Polisi imekuja kukanusha ripoti iliochapishwa kwenye vyombo vya habari nchini humo kwamba polisi imewatia nguvuni watu 4 wanaoshukiwa kuhusika na kifo cha Patrick Karegeya nchini Afrika Kusini.

Mwili wa Karegeya ulikutwa ndani ya chumba kimoja cha Hoteli jijini Johanesbourg huku kukiwa na ishara ya kuuawa kwa kunyongwa.