COTE D'IVOIRE-Siasa

Utawala wa Abidjan umewataka raia wake waishio uhamishoni kurejea nchini kwa ujenzi wa taifa

Rais wa Cote d'Ivoire, Alassane Outtara
Rais wa Cote d'Ivoire, Alassane Outtara RFI

Serikali nchini Cote d'Ivoire imeendelea kutoa wito kwa raia wake wanaoishi uhamishoni kurejea nchini mwao kama alivyoelekeza rais wa taifa hilo, Alassane Outtara kwenye hotuba yake ya mwisho mwa mwaka jana, ambae aliwataka raia waishio ukimbizini kurejea nchini katika hali ya kujiunga na raia wengine kwa ujenzi wa taifa.

Matangazo ya kibiashara

Toka machafuko ya mara baada ya uchaguzi mkuu mwaka 2010-2011, maelfu ya raia waliikimbia nchi yao na kwenda mataifa jirani kuomba hifadhi kuhofia maisha yao kutokana na kutetereka kwa hali ya kisiasa nchini humo kati ya wafuasi wa rais Outtara na aliyekuwa kiongozi wa taifa hilo, Laurent Gbagbo.

Waziri wa mambo ya ndani nchini Cote d'Ivoire, Hamed Bakayoko amesema wakati umefika kwa raia wake waliokimbia nchini humo kurejea nyumbani wakiwemo wanasiasa wa upinzani ambao walikuwa wanahofia kukamatwa mara baada ya kuingia madarakani kwa utawala mpya.

“Tunarejelea ujumbe wa rais ambaye anawaomba wakimbizi wote warejee nchini.

Hayo yote yatafanyika katika mazingira mazuri hata na wapinzani wetu, tungetamani kuwepo na maridhiano ya kweli ili kurejesha amani. Huu sio mkakati wa kisiasa, sio mtego, hatuna budi.

Tunaamini kuwa nchi hii haiwezi kuendelea bila ya maridhiano na muungano katika kazi”, amesema Bakayoko.

Waziri Bakayoko amesema kuwa hatua hii sio ya kisiasa bali inalenga kuleta umoja wa kitaifa kwa kuwashirikisha raia wake katika ujenzi wa taifa lao.