UMOJA WA AFRIKA

Usalama wa DR Congo kutawala mkutano wa AU jijini Addis Ababa

Leo ni siku ya pili na ya mwisho ya mkutano wa viongozi wa Afrika unaoendelea katika Makao Makuu ya Umoja huo jijini Addis Ababa nchini Ethiopia. Viongozi hao pamoja na mambo mengine wanajadili mizozo katika mataifa ya Jamhuri ya Afrika ya Kati na Sudan Kusini na kujaribu kutafuta suluhu la kudumu ili kukomesha vita vilivyosababisha maelfu ya watu kupoteza maisha na wengine kuyakimbia makwao.

Matangazo ya kibiashara

Mbali na mataifa hayo mawili, hali ya Usalama Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo itapewa kipaumbele katika kikao hicho.

Mataifa kumi na moja ya Ukanda wa Maziwa Makuu yaliyosaini makubaliano kuhusu amani na usalama Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, yatathathmini hatua zilizofikiwa, kipindi hiki wataalam wa Umoja wa Mataifa wakisema Rwanda na Uganda wanawahifadhi waasi wa M 23 na wanajipanga upya kuvamia tena Mashariki mwa DR Congo.

Serikali ya Kinsasha inasema bado inasuburi thathmini ya Umoja wa Mataifa katika utekelezwaji wa makubaliano hayo.

Haya yanajiri wakati Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa likipiga kura kuunga mkono mapendekezo ya Kamati inayoshuhgulikia vikwazo katika Umoja huo kuwa kundi la M 23 limeanza kujipanga upya, na linapewa mafunzo na kufadhiliwa na Rwanda pamoja na Uganda.

Licha ya Rwanda kuunga mkono mapendekezo hayo, Balozi wake katika Baraza hilo la Umoja wa Mataifa Eugene-Richard Gasana amesema ripoti hiyo si ya kweli na kuifananisha Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kama mtoto mdogo anayependa kulia na kulalamika kila mara.

Naye Balozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Ignace Gata Mativa amesema kuwa ripoti ya Kamati hiyo imeonesha wazi namana Rwanda na Uganda wanavyosababisha ukosefu wa usalama Mashariki mwa DR Congo.

Nchi za Rwanda na Uganda zimeendelea kukanusha tuhma hizo za kulisaidia kundi la M 23.