SUDANI KUSINI-Mazungumzo

Navi Pillay anaendelea na ziara yake nchini Sudani Kusini

Navi Pillay, mkuu wa masuala ya haki za binadamu kwenye Umoja wa Mataifa.
Navi Pillay, mkuu wa masuala ya haki za binadamu kwenye Umoja wa Mataifa. REUTERS/Dinuka Liyanawatte

Mazungumzo ya amani kati ya waasi na serikali ya Sudan Kusini kwa siku ya pili yanaendelea leo jijini Addis Ababa nchini Ethiopia ili kujaribu kupata ufumbuzi wa kisiasa katika mzozo unaosababisha mauaji kuongezeka katika taifa hilo changa tangu desemba 15.

Matangazo ya kibiashara

Lengo ni kujaribu kupata muafaka wa kumaliza mzozo wa miezi minne sasa kati ya waasi wanaongozwa na aliyekuwa makamu wa rais Riek Machar na majeshi ya rais Salva Kiir, mzozo ambao umesabisha maelfu ya raia kupoteza maisha na wengine kukimbia makwao.

Mazungumzo hayo yanaongozwa na muungano wa nchi za IGAD unaolenga kupata muafaka wa kisiasa na maridhiano.

Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya siasa wanaona kwamba mazungumzo hayatazaa matunda, kwa sababu hayajawahi kufaanikiwa tangu yalipoanza.

Wakati hayo yakijiri mkuu wa masuala ya haki za binadamu kwenye Umoja wa Mataifa Navi Pillay, ambaye aliombwa na Baraza la Usalama la umoja wa Mataifa kufanya uchunguzi kuhusu mauaji nchini Sudani Kusini, anaendelea na ziara yake.

Afisa huyo wa ngazi ya juu kwenye Umoja wa Mataifa anatarajiwa kutembelea eneo linaloshikiliwa na waasi ambao wanapigana tangu desemba 15 na jeshi la Sudani Kusini linaomuunga mkono rais wa nchi hio Salva Kiir.

Machafuko hayo yamesababisha maefu ya raia kupoteza maisha na wengine zaidi ya 400.000 wameyahama makaazi yao tangu yalipoanza desemba 15.