Nigeria: watu 18 wauwa katika shambulio la bomu mjini Abuja
Imechapishwa:
Watu 18 wamepoteza maisha na zaidi ya 80 wamejeruhiwa baada ya bomu lililokuwa limetegwa ndani ya gari dogo kulipuka katika mji mkuu wa Nigeria, Abuja, Idara ya shughuli za uokozi imethibitisha.
Mlipuko huo umetokea saa mbili saa za kimataifa usiku wa jana katika ktuo cha magari cha Nyanya, kwenye umbali wa mita 50 na eneo kulikotokea mlipuko mwengine aprili 14, shambulio liliodaiwa kutekelezwa na wanamgambo wa kislamu wa kundi la Boko Haram, ambalo liliwaua watu 75 na makumi wengine kujeruhiwa.
Mashahidi wanasema, shambulio hilo liliwalenga maafisa wa polisi waliokuwa wanalinda kizuizi cha kuingia katika kituo hicho cha mabasi.
Hadi sasa hakuna kundi lililojitokeza na kudai kutekeleza shambulio hilo, lakini mwezi uliopita kundi la wanamgambo wa kislamu la Boko Haram lilikiri kushmabulia kituo hicho cha mabasi.
Kutokea kwa mashambulizi haya jijini Abuja, kumeanza kuzua wasiwasi wa kundi hilo lenye makaazi yake kaskazini mwa nchi hiyo , ambalo limeanza kuulenga mji mkuu wa taifa hilo.
Shamabulio hili linakuja juma moja kabla ya kufanyika kwa mkutano wa kimataifa wa kiuchumi, mjini Abuja na polisi wanasema watahakikisha kuwa wageni wanakuwa katika salama thabiti.
Mbali na hilo jeshi nchini humo limeendelea kuwatafuta zaidi ya wasichana 200 waliotkewa nyara na watu wasiojulikana wakiwa shuleni mwezi uliopita katika jimbo la Borno.