Sudani Kusini: Mapigano yarindima karibu na mji wa Bentiu
Imechapishwa: Imehaririwa:
Mapigano yameendelea leo katika mji mkuu wa jimbo la Unity, Bentiu (kaskazini mashariki), ambapo jeshi la Sudani Kusini linajaribu kuurejesha mji huo kwenye himaya yake, tangu waasi wanaomuunga mkono Rieka Machar kuudhibiti, licha ya mazungumzo ya amani yanayoendelea katika mji wa Addis Ababa, Ethiopia.
“Tunapigana ndani na kando ya mji wa Bentiu ili kuurejesha mji huo kwenye himaya yetu”, amesema msemaji wa jeshi la Sudani Kusini Philip Aguer, huku akibaini kwamba licha ya waasi kujidhatiti wataurejesha tu kwenye himaya yao.
Jeshi la Sudani Kusini lilitangaza jana kwamba limeingia katiaka mji wa Bentiu, na kuna shahidi ambae alifahamisha shirika la habari la Ufaransa AFP kwamba jeshi linaelekea kuwa limeurejesha kwenye himaya yake mji wa Bentiu.
Waasi wanaoongozwa na Riek Machar, ambaye alin'gatuliwa mwezi julai mwaka 2013 na rais Salva Kiir, waliendesha mashambulizi katikati ya mwezi wa aprili, na kuuteka mji wa Bentiu, ambao ulitekwa mara kadhaa na waasi hao tangu mapigano yalipozuka nchini Sudani Kusini katikati ya mwezi wa desemba kati ya jeshi linalomuunga mkono rais Salva Kiir na Riek Machar kutokana na malumbano yao ya kisiasa.
Malumbano hayo ya kisiasa yenye misingi ya kikabila kati ya watu kutoka jamii za Dinka (kabila la Salva Kiir) na Nuer (kabila la Machar), na kusababisha machafuko yaliyosababisha maelfu ya raia kuuawa na maelfu wengine kuyahama makaazi yao.
Hayo yakijiri waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani John Kerry, ametoa onyo kali kwa pande zinazohusika na mgogoro nchini sudani Kusini kutekeleza ahadi zao za kusitisha mapigano, na kubaini kwamba upande wowote utakaokataa kutia silaha chini utachukuliwa vikwazo ambavyo vitaupelekea hata kuwa katika maisha magumu.
Kerry ameyasema hayo katika mkutano na waandisha wa habari mjini Luanda nchini Angola, anakohitimisha ziara yake ya siku 6 barani Afrika.