AFRIKA KUSINI-Uchaguzi

Raia wanapiga kura Afrika Kusini

Raia wa Afrika Kusini wakisubiri kufunguliwa kwa vituo vya kupigia kura mapema leo asubuhi katika kitongoji kimoja cha Johannesburg, mei 7 mwaka 2014.
Raia wa Afrika Kusini wakisubiri kufunguliwa kwa vituo vya kupigia kura mapema leo asubuhi katika kitongoji kimoja cha Johannesburg, mei 7 mwaka 2014. RFI / Alexandra Brangeon

Zaidi ya wapiga kura milioni 25 wa Afrika Kusini wanatarajiwa kuwachagua wabunge 400 ambao watamchagua baadae rais katika uchaguzi mkuu ujao utakaofanyika tarehe 21 mwezi huu.

Matangazo ya kibiashara

Uchaguzi huo wa wabunge ni moja ya chaguzi zilizogubikwa na changamoto kadhaa katika muktadha wa mvutano wa kijamii uliojitokeza hivi karibuni nchini humo kukiwepo maandamano na vurugu dhidi ya kile kilichoitajwa uzembe wa viongozi kutoka chama tawala cha ANC.

Hata hivyo, kura ya maoni iliyofanyika na Taasisi ya Mafunzo ya Usalama ISS na kutangazwa jana, imebaini kuwa licha ya kuwa chama tawala cha ANC kinatarajiwa kushinda kwa asilimia 60 %, huenda kikapoteza maeneo mengi ikilinganishwa na mwaka 2009.

Vyama vya upinzani vinavyokiletea changamoto chama hicho ni chama cha Democratic Alliance na chama kichanga cha Freedom Economic Fighters cha Julius Malema, mwenye umri wa miaka 33 na mgeni wa mazingira ya chaguzi za kisiasa nchini humo.

Hadi dakika ya mwisho , vyombo vya usalama nchini humo vimerudia wito wao kwa wananchi wa Afrika kusini kwa ajili ya utulivu siku ya uchaguzi, wakati maandamano ya vurugu katika makazi duni na vitongoji maskini vinafanyika kila kukicha, hasa katika vitongoji vya Johannesburg na Cape Town.

Miaka mitano ya awamu ya kwanza ya rais Zuma imegubikwa na kashfa kadhaa, ya mwisho ikiwa ile ya ukarabati wa makazi yake binafsi wilaya ya Nkandla ambapo ametuhumiwa kutumia fedha za walipakodi bila kusahau mauwaji yaliyofanyika na polisi kwenye mgodi wa Marikana mwezi Agosti mwaka 2012, na kusababisha vifo vya watu 34.