SUDANI KUSINI-UN-MAzungumzo

Sudani Kusini: Riek Machar yuko tayari kukutana na Salva Kiir

Makamu wa zamani wa rais nchini Sudani Kusini, Machar amesema yuko tayari kushiriki mazungumzo mjini Addis Ababa, nchini Ethiopia.
Makamu wa zamani wa rais nchini Sudani Kusini, Machar amesema yuko tayari kushiriki mazungumzo mjini Addis Ababa, nchini Ethiopia. REUTERS/Goran Tomasevic

Kiongozi wa kundi la waasi wa Sudan Kusini, Riek Machar ameahidi kuwa atashiriki mazungumzo ya amani mjini Addis Ababa, Ethiopia kujaribu kusitisha vita viliyolikumba moja kati ya mataifa mapya zaidi duniani, wakati huu ambapo serikali ya Marekani ikitangaza vikwazo dhidi ya viongozi wa Sudan Kusini.

Matangazo ya kibiashara

Akiwa ziarani kwenye nchi hiyo, katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa UN, Ban Ki Moon amezitaka pande mbili zinazokinzana nchini humo kukubali na kukutana ana kwa ana mjini Addis Ababa kuzungumzia mzozo wa taifa hilo ili kunusuru vifo zaidi vya wananchi wasio na hatia.

Rais wa Sudani Kusini, Salva Kiir.
Rais wa Sudani Kusini, Salva Kiir. REUTERS/Andreea Campeanu

Akizungumza mara baada ya kukutana na katibu mkuu Ban Ki Moon, rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir amemuahidi kiongozi huyo kuwa yuko tayari kwenda Juba kukutana na mwenzake iwapo naye atafanya hivyo.

Kwa upande wake Katibu Mkuu

Ban, anasema kuwa amefanya kila linalowezekana kuwashawishi viongozi hawa na kwamba alizungumza kwa njia ya simu na Riek Machar na kumpa hakikisho la kuhudhuria mazungumzo ya amani mjini Addis Ababa, Ethiopia.

Hatua hii inafikiwa huku nchi ya Marekani hapo jana ikitangaza vikwazo dhidi ya Marial Chanuong kamanda wa kikosi maalumu cha rais pamoja na Peter Gadet kiongozi wa kundi la wapiganaji wanaopinga uasi kwenye nchi hiyo.

Mapigano kati ya jeshi linalomuunga mkono raia Salva Kiir na waasi wanao muunga mkono, Riek Machar, aliekua makamu wa Salva Kiir, yamesababisha vifo vya maelfu ya watu huku watu zaidi ya 500.000 wakihama makaazi yao.