UGANDA-Mapenzi ya jinsia moja-Sheria

Uganda: watuhumiwa wa mapenzi ya jinsia moja wafikishwa mahakamani

Wanaharakati wanaotetea ndoa za jinsia moja wakipinga sheria inayopiga marufuku ndoa za jinsia moja mjini Kampala, nchini Uganda.
Wanaharakati wanaotetea ndoa za jinsia moja wakipinga sheria inayopiga marufuku ndoa za jinsia moja mjini Kampala, nchini Uganda. REUTERS/Edward Echwalu

Watu wawili wanaodaiwa kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja, hapo jana wamefikishwa kwenye mahakama moja nchini Uganda, ikiwa ni kesi ya kwanza kuanza kusikilizwa toka kusainiwa kwa sheria kali inayokataza mapenzi ya jinsia moja.

Matangazo ya kibiashara

 

Watuhumiwa hao, Kim Mukisa na Jackson Mukasa wote kwa pamoja wamekana kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja, kwenye kesi ambayo tayari imevuta hisia za watu wengi hasa wanaharakati wanaopinga sheria iliyopitishwa na Serikali.

Licha ya kuwa baadhi ya kesi kama hizo ambazo zimewahi kusikilizwa kwenye mahakama za mjini Kampala na kufutwa kutokana na kukosekana kwa ushahidi, safari hii upande wa mashtaka unasema inao ushahidi kuthibitisha watu hao kujihusisha na vitendo hivyo.

Rais wa Uganda Yoweri Museveniakisaini sheria inayopiga marufuku mapenzi ya jinsia moja. in Entebbe
Rais wa Uganda Yoweri Museveniakisaini sheria inayopiga marufuku mapenzi ya jinsia moja. in Entebbe Reuters/James Akena

Mwezi February mwaka huu rais wa Uganda, Yoweri Museveni alitia saini na kuwa sheria muswada uliowasilishwa kwake na bunge ambao unakataza ndoa za watu wa jinsia moja na kwamba atakayepatikana na hatia atakabiliwa na kifungo cha maisha jela.

Kutiwa saini kwa sheria hiyo kulishuhidia hata baadhi ya mataifa ya magharibi ambayo ni wafadhili wa nchi ya Uganda wakisitisha misaada yao kwa kile wanachodai sheria hiyo inaminya uhuru wa watu na kwamba rais Museveni ametia saini ili ajipatie umaarufu kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2016.