NIGERIA-Usalama

Goodluck: wasichana waliyotekwa watapatikana

Rais wa Nigeria, Goodluck Jonathan
Rais wa Nigeria, Goodluck Jonathan Reuters/Tiksa Negeri/Files

Wakati nchi za Marekani, Uingereza, Uchina na Ufaransa zikiwa zimeungana na nchi ya Nigeria katika operesheni maalumu ya kuwasaka wasichana waliotekwa na kundi la Boko Haram, rais wa Nigeria Goodluck Jonathan amesisitiza kuwa wasichana hao watapatikana na kurejea kwenye familia zao.

Matangazo ya kibiashara

Rais Jonathan ameyasema hayo kando na mkutano wa Jukwaa la kiuchumi unaofanyika nchini Nigeria, ambapo amesema kuwa mpaka sasa hawajaweza kubaini ni kitu gani kilitokea wakati wa tukio lenyewe lakini wana imani kwamba kwa msaada wanaoupata hivi sasa watafanikiwa kujua.

Familia za wanafunzi wasichana waliyotekwa nyara na kundi la Boko Haram nchini Nigeria.
Familia za wanafunzi wasichana waliyotekwa nyara na kundi la Boko Haram nchini Nigeria. REUTERS/Stringer

Rais Jonathan ametumia mkutano huu kuzishawishi nchi za Afrika na Dunia kwa ujumla kuendelea kuungana katika harakati za kupiga vita vitendo vya Ugaidi na kwamba vikiachiwa kuendelea vitahatarisha usalama wa nchi na kurudisha nyuma maendeleo ya nchi.

Katika hatua nyingine utafiti uliofanywa hivi karibuni kuhusu kundi la Boko Haram, unaonesha kuwa kiongozi wa sasa wa kundi hilo, Abubakar Muhammad Shekau ameligeuza kundi hilo kuwa hatari zaidi kuliko lilivyokuwa hapo awali, hali inayoashiria kuwa kuna kazi ya ziada kudhibiti shughuli zake.