UN-SUDANI KUSINI-Uhalifu

UN: uhalifu dhidi ya binadamu katika machafuko nchini Sudani Kusini

Ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu nchini Sudan Kusini, imeonyesha kuwa kuna uwezekano mkubwa wa pende zinazokinzana kwenye mzozo wa taifa hilo kuhusika na makosa ya uhalifu dhidi ya binadamu.

Wakimbizi wa ndani wa Sudani Kusini wakipewa hifadhi katika kambi ya umoja wa Mataifa ya Jabel, nchini Sudani.
Wakimbizi wa ndani wa Sudani Kusini wakipewa hifadhi katika kambi ya umoja wa Mataifa ya Jabel, nchini Sudani. REUTERS/James Akena
Matangazo ya kibiashara

Ripoti hii ya Umoja wa Mataifa inatolewa wakati huu ambapo hii leo rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir anatarajiwa kukutana ana kwa ana kwa mara ya kwanza toka kuanza kwa machafuko nchini humo na aliyekuwa makamu wake wa rais Riek Machar mjini Addis Ababa Ethiopia.

Umoja wa mataifa nchini Sudan Kusini unasema kuwa kuna kila aina ya vidhibiti ambavyo vinaonesha kuwa ni wazi kulikuwa na vitendo vya makosa ya uhalifu dhidi ya binadamu yaliyofanywa na upande wa serikali na ule wa waasi wanaoongozwa na Riek Machar.

kikosi cha wanajeshi wa Umoja wa Mataifa kikiwalindia usalama raia nchini Sudani Kusini.
kikosi cha wanajeshi wa Umoja wa Mataifa kikiwalindia usalama raia nchini Sudani Kusini. REUTERS/UNMISS/Handout via Reuters

Kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa, makosa hayo ya uhalifu wa binadamu yanahusiana na mauaji, kupotezwa kwa baadhi ya watu, ukiukwaji wa haki za binadamu, ubakaji, na kukamatwa kiholela bila kuheshimu sheria.

Umoja wa Mataifa umebaini kwamba kuna mashambulizi yaliyowalenga raia wasiyo kua na hatia, hata hospitali zililengwa na pande zote mbili zinazokinzana.

Kwa upande wake ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini Sudani Kusini imefahamisha kwamba baadhi ya raia walilengwa kutokana na tofauti zao za kikabila, huku ikibaini kwamba pande zote husika katika mgogoro unaoendelea zilihusika katika visa mbalimbali vya ukiukwaji wa haki za binadamu na ubakaji dhidi ya wanawake kutoka jamii tofauti.

Wakati huohuo, shirika la kimataifa linalotetea haki za binadamu Amnesty international limetoa onyo kwa viongozi wa pande hizo mbili kuwachukulia hatua za kisheria wanajeshi na waasi waliyohusika na makosa hayo akiwataka kuwa na majukumu kwa wapiganaji wao.