NIGERIA-BOKO HARAM-Usalama

Nigeria na nchi jirani zaapa kupambana na Boko Haram

Marais wa Nigeria, Chad,Cameroon, Niger na Benini  pamoja na rais wa Ufaransa katika picha ya pamoja jijini Paris
Marais wa Nigeria, Chad,Cameroon, Niger na Benini pamoja na rais wa Ufaransa katika picha ya pamoja jijini Paris REUTERS/Gonzalo Fuentes

Serikali ya Nigeria na majirani zake zimeapa kuunganisha vikosi vya kijeshi dhidi ya kundi la Boko Haram chini ya mkataba unaotambulika kama tamko la vita dhidi ya wanamgambo wa Kiislam wanaowashikilia wasichana wa shule zaidi ya 200.

Matangazo ya kibiashara

Wakikutana mjini Paris Ufaransa , Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan na wenzake wa Benin, Chad, Cameroon na Niger wamepitisha mpango mkakati wa kukabiliana na kundi hilo ambalo linatuhumiwa kwa vifo vya watu 2000 kwa mwaka huu na utekaji wa wasicha na zaidi ya 200 mwezi uliopita Kaskazini Mashariki mwa Nigeria.

Akizungumza katika mkutano huo rais wa Ufaransa Francois Hollande amesema kuwa kundi la Boko Haram linauhusiano na kundi la kigaidi la Al qaeda hivyo mbinu za kikanda zinahitajika ili kudhibiti kundi hilo.

Hayo yanajiri huku kundi hilo likituhumiwa kutekeleza shambulio jingine wakati mkutano wa viongozi wa hao ukiendelea na kumwua askari mmoja wa Cameroon na kuwateka nyara wafanyakazi 10 wa barabara raia wa China.

Wanamgambo hao walivamia kambi inayotumiwa na wafanyakazi wa barabara raia wa China Ijumaa usiku katika mkoa wa kaskazini mwa Cameroon karibu na mpaka wa ngome ambapo waliwateka zaidi ya wasichana 200 mwezi uliopita.