MALAWI-Uchaguzi

Malawi: zoezi la kupiga kura laendelea

Rais anaeondoka madarakani Joyce Banda akipiga kura katika kituo cha kupigia kura cha Malemia, nchini Malawi.
Rais anaeondoka madarakani Joyce Banda akipiga kura katika kituo cha kupigia kura cha Malemia, nchini Malawi. REUTERS/Eldson Chagara

Zoezi la kupiga kura limeendelea leo jumatatu katika baadhi ya vituo vya kupigia kura nchini Malawi, siku moja baada ya uchaguzi wa urais, wa bunge pamoja na wa madiwani kufanyika.

Matangazo ya kibiashara

Uchaguzi huo umegubikwa na maandamano pamoja na machafuko yaliyotokana na uchaguzi ambao unadaiwa kuandaliwa vibaya.
Baadhi ya vituo vya kupigia kura vimefungua kwa kuchelewa kwa saa 10, na kusababisha hasira na minongono miongoni mwa raia.

Vituo vya kupigia kura 13 kwa jumla ya vituo 4.475, ambako nyaraka za uchaguzi zilichomwa na sehemu nyingine kutokea vurugu, kwa mujibu wa tume ya uchaguzi, vituo hivyo vimefunguliwa saa moja asubuhi saa za Afrika ya mashariki na kufungwa saa kumi na moja jioni. Zoezi hili la kupiga kura limecheleweshwa kwa mara nyingine tena katika kituo kimoja cha kupigia kura cha Blantyre.

Mkuu wa tume ya uchaguzi, Maxon Bendera, ameomba radhi kufuatia hali hio, huku akisema kwamba hakupendelea kuona raia wa Malawi wananyimwa haki yao ya msingi ya kupiga kura. Ameomba pia kutumwa kwa wanajeshi kwenye vituo hivyo ili kusaidia polisi kulinda usalama.

Zoezi hili la chaguzi tatu kwa pamoja ni kipimo cha cha hali ya juu kwa rais anaeondoka madarakani Joyce Banda, mwenye umri wa miaka 64, ambaye aliwasili madarakani bila kuchaguliwa, baada ya kifo cha rais Bingu wa Mutharika.

Wagombea 12 wanawania kiti cha urais, lakini wanne ndio wanaongoza, akiwemo rais Joyce Banda, ambaye anapewa nafasi kubwa ya kushinda kutokana na kuwa wapinzani wake hawakushikamana kwa pamoja ili wawe na kura nyingi za pamoja.

Serikali ya Joyce Banda ilikosolewa vikali kutokana na kashfa ya ufisadi, lakini rais huyo alijitetea na kusema kwamba watu waliyohusika na kashfa ya ufisadi walikamatwa baada ya kuunda tume ya uchunguzi kuhusu kashfa hio.

Mpizani mkuu wa Banda ni Peter Mutharika, mwenye umri wa miaka 74, ndugu wa hayati rais Bingu wa Mutharika.

Na mwengine ambae anaonekana kuongoza katika uchaguzi huo, kwa mujibu wa waangalizi ni mwanaye rais wa zamani Bakili Muluzi, Atupele Muluzi, mwenye Umri wa miaka 39, na Lazarus Chakwera, mwenye umri wa miaka 59, ambae ni kiongozi wa chama cha rais wa zamani wa Malawi Kamuzu Banda.

Matokeo yanasubiriwa juma lijalo.