MISRI

Al-Sisi anaelekea kupata ushindi mkubwa nchini Misri

Abdel Fatah al-Sisi
Abdel Fatah al-Sisi Reuters

Aliyekuwa kiongozi wa jeshi nchini Misri Abdel Fattah al-Sisi anaelekea kupata ushindi mkubwa katika Uchaguzi wa Urais uliomaliza siku ya Jumatano juma hili.

Matangazo ya kibiashara

Matokeo ya awali yaliyotangazwa na tume ya Uchaguzi yanaonesha kuwa Al Sisi tayari amepata asilimia 96 nukta 2 ya kura zilizopigwa na wananchi wa taifa hilo.

Hadi sasa, kura katika vituo 312 kati ya 352 zimehesabiwa na mpinzani wa Al Sisi Hamdeen Sabbahi, yeye amepata asilimia 3 nukta 8.

Imekuwa ikitarajiwa kuwa kiongozi huyo wa zamani wa jeshi aliyemwondoa rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia Mohammed Morsi mwaka uliopita atashinda uchaguzi huo.

Wachambuzi wa siasa wanaona kuwa hakuna kipya kinachotarajiwa kutoka kwa Al-sisi ambaye ataendelea kuongoza nchi hiyo kijeshi.

Wafuasi wa Al Sisi wameonekana katika barabara za jiji la Cairo wakisherehekea ushindi huo ambao wanasema utasaidia kuweka udhabiti wa kisiasa nchini humo.

Hata hivyo, tume ya Uchaguzi unasema ni asilimia 37 ya wapiga kura ndio waliojitokeza kushiriki katika Uchaguzi huo wa urais ikilinganiswa na asilimia 52 mwaka 2012 wakati Morsi alipochaguliwa.

Vijana wengi nchini humo na wafuasi wa kundi lililopigwa marufuku la Muslim Brotherhood hawakupiga kura  kwa kile walichokisema hakukuwa na haja kwa sababu mshindi alishapatikana hata kabla ya kupiga kura.

Hadi sasa hakuna anayefahamu sera ya Al Sisi ambaye wananchi wengi nchini humo wanasema kiongozi huyo wa zamani wa jeshi amekuja kuikoa nchi hiyo.