MALAWI

Matokeo ya urais nchini Malawi huenda yakatangazwa Ijumaa

Upigaji kura nchini Malawi
Upigaji kura nchini Malawi

Matokeo rasmi ya urais nchini Malawi huenda yakatangazwa hapo kesho siku ya  Ijumaa iwapo tu mahakama kuu itabatilisha zoezi la uhesabuji upya wa kura, tume ya taifa ya uchaguzi nchini humo imesema.

Matangazo ya kibiashara

Tume ya uchaguzi siku ya Jumatano  usiku mjini Blantyre, ilisema wameamua kutangaza matokeo hayo kwa kuzingatia sheria inayoibana kufanya hivyo ndani ya siku zisizozidi nane  baada ya saa 48 tangu kumaliza hesabu ya kura.

Uchaguzi wa Malawi uliingia dosari juma lililopita kufuatia rais anayemaliza muda wake Joyce Banda kudai kuwa uchaguzi huo ulikuwa na mapungufu na hasa wizi wa kura uliofanywa na upinzani.

Mahakama nchini humo zimekuwa zikitoa maamuzi tofauti kuhusiana na uchaguzi huo ambapo sasa mahakama kuu inasubiriwa kuamua iwapo tume itangaze matokeo ya awali yaliyokuwa yamekamilika au kusbiri matokeo mengine baada ya kura kuhesabiwa upya.

Iwapo uamuzi huu utatolewa  tume ya taifa ya uchaguzi nchini humo itatangaza matokeo rasmi hapo kesho, wakati huu wafuasi wa Peter Mutharika wakishinikiza kutangazwa kwa matokeo haya.

Chama cha PDP kimetangaza Kamati ya kumwapisha kiongozi wa chama hicho Peter Mutharika, kwa kile ambacho chama hiki kinasema ameshinda Uchaguzi huu.

Kabla ya kura kuanza kuhesabiwa, Mutharika alikuwa anaongoza kwa mujibu wa matokeo ya awali yaliyokuwa yanatangazwa na tume ya Uchaguzi kabla ya rais Joyce Banda aliyekuwa wa tatu kujitokeza na kudai wizi wa kura na hata kuagiza kufutilia mbali Uchaguzi huo lakini Mahakama ikabadilisha.

Wananchi wa Malawi wamejikuta katika njia panda kuhusu matokeo ya Uchaguzi huo ambao huenda yakatangazwa siku ya Ijumaa ikiwa Mahakama itaamua kura kuhesabiwa upya.