KENYA

Kenyatta: Tutazungumza na upinzani lakini sio kuunda Serikali ya pamoja

Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta akizungumza wakati wa sherehe za madaraka day juma hili
Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta akizungumza wakati wa sherehe za madaraka day juma hili Kenyagvt

Rais wa Kenya, Uhuru Mwigai Kenyatta amesisitiza kuwa Serikali yake iko tayari kufanya mazungumzo na viongozi wa upinzani lakini akakanusha utawala wake kuwa tayari kuunda Serikali ya pamoja na viongozi hao. 

Matangazo ya kibiashara

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta akiwa na naibu wake, William Ruto
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta akiwa na naibu wake, William Ruto Reuters/Presidential Strategic Communications Unit

Rais Kenyatta ametoa kauli hiyo wakati wa maadhimisho ya sherehe za Madaraka day kutimiza miaka 51 toka nchi hiyo ijitawale, ambapo amesema kuwa yuko tayari kwa mazungumzo na upinzani lakini hayuko tayari kuunda Serikali ya kitaifa.

Kauli ya rais Kenyatta imekuja baada ya siku ya Jumamosi muungano wa kisiasa wa CORD kumtaka kiongozi huyo kukutana nao tarehe 7 ya mwezi wa 7 mwaka huu kwaajili ya mazungumzo na kuunda Serikali ya pamoja.

Akiwahutubia maelfu ya wafuasi wa muungano huo baada ya kurejea nyumbani, kinara wa muungano huo, Raila Odinga amesema kuwa ni lazima Serikali ya Jubilee ikubaliane na matakwa yao ama sivyo wajiandae kuondoka madarakani.

Kauli hiyo ndio iliyomfanya rais Kenyatta wakati wa hotuba yake kwa wananchi wakati wa maadhimisho ya miaka 51 ya Madaraka Day kutamka hadharani kuwa yuko tayari kwa mazungumzo na wanasiasa wa CORD kuhusu mustakabali wa taifa hilo lakini akatupilia mbali uwezekano wa serikali yake kuunda Serikali ya pamoja.

Kinara wa muungano wa kisiasa wa CORD, Raila Odinga
Kinara wa muungano wa kisiasa wa CORD, Raila Odinga RFI

Rais Kenyatta amesema Serikali yake licha ya kukabiliwa na changamoto za kiusalama, bado iko imara na kwamba hakuna haja ya kuwa na Serikali ya pamoja na wanasiasa wa upinzani na kuwakejeli kuwa wasipende vya kupewa na badala yake wasibiri uchaguzi mwingine.

Muungano wa CORD unadai kuwa Serikali ya Jubilee imeshindwa kuongoza taifa hilo na kwamba kumekuwa na matukio mengi yanayohatarisha usalama wa nchi na kwamba nchi pekee ni kuwa na Serikali ya pamoja ama ijiondoe madarakani.

Kwa upande wake kinara wa chama cha Wiper na aliyekuwa makamu wa rais, Kalonzo Musyoka amesema kuwa ili taifa hilo lirejee kwenye umoja wa kitaifa ni lazima kuwe na Serikali ya kitaifa wakati huu ambapo hali ya usalama imeendelea kuzorota.

Aliyewahi kuwa makamu wa rais wa Kenya, Kalonzo Musyoka ambaye sasa yuko kwenye muungano wa CORD
Aliyewahi kuwa makamu wa rais wa Kenya, Kalonzo Musyoka ambaye sasa yuko kwenye muungano wa CORD http://twanatwitucares.org/

Kauli ya wanasiasa wa CORD imekosolewa pakubwa na wabunge wa Jubilee ambao wamedai muungano huo unataka kuhatarisha usalama wa nchi kwa kutaka kuitisha maandamano ya kushinikiza utawala wa rais Kenyatta kuondoka madarakani kabla ya muda.

Kufuatia kauli ya rais Kenyatta sasa inasubiriwa kuona aina ya mazungumzo ambayo viongozi wa Muungano wa CORD na wale wa Jubilee watayafanya ili kufikia suluhu ya kisiasa nchini Kenya.