NIGERIA-Maandamano

Vijana wa Jimbo la Kano waandamana kupinga uteuzi wa mfalme wa jimbo hilo

Maandamano ya watu wa nigeria
Maandamano ya watu wa nigeria l'express

Maelfu ya vijana nchini Nigeria wameandamana kwenye mji wa pili kwa ukubwa nchini humo wa Kano, kupinga kutangazwa kwa aliyekuwa gavana wa benki kuu ya nchi hiyo kama mfalme wa jimbo hilo. 

Matangazo ya kibiashara

Maandamano hayo yamefanyika saa chache tu baada ya utawala wa Jimbo la Kano, kumtangaza aliyekuwa gavana wa benki kuu ya nchi hiyo, Sanusi Lamido kuwa mfalme wa jimbo hilo akiziba nafasi ya mfalme Ado Abdullahi Bayero aliyefariki mwishoni mwa juma lililopita.

Kufuatia kutangazwa kwa Sanusi kama mfalme wa eneo hilo, mamia ya vijana waliandamana kwenye jimbo hilo wakipinga gavana huyo kutangazwa kiongozi wao na kuanza kurusha mawe na kuchoma moto matairi nje ya ofisi za gavana wa jimbo hilo.

Vijana hao wanataka mtoto mkubwa wa aliyekuwa kiongozi wao, Aminu Ado Bayero arithi nafasi ya baba yake kuliko Gavana Sanusi ambaye hivi karibuni alifutwa kazi na rais Goodluck Jonathan kwa tuhuma za rushwa.

Wachambuzi wa mambo wanaona kuwa uteuzi wa Sanusi ambaye alikuwa ni mjukuu wa mfalme aliyefariki juma lililopita umefanywa kisiasa kwa lengo la kuendelea kumjengea umaarufu na kutaka kumlinda dhidi ya Serikali pamoja na matamshi yake ya kuikosoa Serikali yake.

Mfalme wa jimbo la Kano ni cheo cha pili kwa ukubwa nyuma ya kiongozi wa kiislamu kwenye taifa hilo na pia mfalme wa Sokoto na shehu wa jimbo la borno, vyeo ambavyo vimekuwepo toka wakati wa utawala wa kikoloni.