UGANDA

Uganda yasikitishwa na vikwazo ilivyowekewa na Marekani

Rais wa Uganda Yoweri Museveni
Rais wa Uganda Yoweri Museveni Reuters/James Akena

Serikali ya Uganda inasema vikwazo ilivyowekewa na serikali ya Marekani kutokana na sheria iliyotiwa saini na rais Yoweri Museveni mapema mwaka huu kuharamisha vitendo na mapenzi ya jinsia moja nchini humo, vitawaumiza wananchi wa kawaida.

Matangazo ya kibiashara

Juma lililopita, Marekani ilitangaza kusitisha mafunzo ya jeshi la angaa kwa jeshi la Uganda pamoja na kusitisha misaada ya kibinadamu ikiwemo, kuwazuia viongozi kadhaa wa serikali ya Kampala kuzuru Marekani.

Wizara ya mambo ya nje nchini Uganda inasema, imeshangazwa na kusikitishwa mno na hatua hiyo ya Marekani kwa kile inachosema inawaumiza raia wake wasiokuwa na hatia.

Licha ya lalama hizo, serikali ya Kampala inasema uhusiano wake na Washington DC utasalia kuwa mzuri na watashirkiana na nchi hiyo katika maswala mengine likiwemo swala la kumtafuta kiongozi wa kundi la waasi la LRA Joseph Kony.

Kabla ya kutangaza vikwazo hivyo, Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani John Kerry alisema sheria hiyo dhidi ya wapenzi wa jisnia moja inafafana na sera ya uongozi wa Kinazi nchini Ujerumani wakati wa Vita vya dunia.

Wanaharakati wa mapenzi ya Jinsia moja nchini Uganda, wamekuwa wakiyaomba mataifa ya Magharibi yakiongozwa na Marekani kumshawishi rais Museveni kubadilisha sheria hiyo bila ya mafanikio.

Mashirika ya kutetea haki za Binadamu yakiongozwa na lile la Human Rights Watch yameendelea kuishtumu serikali ya Uganda kwa kupitsiha sheria hiyo wanayosema inawabagua watu hao kitu wanachoeleza ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.

Rais Yoweri Museveni wakati akiitia saini sheria hiyo mpya alisema alichukua hatua hiyo, ili kulinda maadili ya raia wa Uganda na waafrika.

Yeyote anayekamatwa akishiriki vitendo vya mapenzi ya jinsia moja atafungwa jela maisha.