EQUITORIAL GUINEA

Ban kwa viongozi wa Afrika: Heshimuni haki ya kujieleza

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon amewahotubia viongozi wa Afrika jijini Malabo nchini Equitorial Guinea na kuwataka kuheshimu haki ya kujieleza.

Matangazo ya kibiashara

Hotuba ya Moon ililimlenga rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi na kumwomba awaachilie huru wanahabari watatu wa Al Jazeera waliohukumiwa miaka 7 jela juma hili kwa kosa la kushirikiana na kundi lililoharamishwa la MuslimBrotherhood na kutangaza habari za kupotosha.

“Naomba nchi zote ikiwemo Misri, kuheshimu haki ya kujieleza na haki ya kupata habari kutoka kwa waandishi wa Habari,” alisema.

“Nimekutana na rais Sisi hapa Malabo na tumejadili kwa kina kuhusu suala hili, na nimemuomba aheshimu haki ya kujieleza,” aliongezea.

Rais Abdel Fattah al-Sisi
Rais Abdel Fattah al-Sisi

Rais Sisi amewashukuru Umoja huo kwa kuirejesha nchi yake katika Umoja huo baada ya kufungiwa kwa mwaka mmoja uliopita kutokana na uongozi wa kijeshi katika taifa lake.

Rais huyo amewaambia viongozi wenzake kuwa Misri, imeanza kupiga hatua kidemokrasia baada ya Uchaguzi wa urais na upitishwaji wa katiba mpya.

“ Naamini kuwa ndugu zangu Waafrika wameamini sasa kuwa mapinduzi ya Juni 30 mwaka uliopita hayakuwa ya kijeshi bali ya wananchi wenyewe,” amesisitiza.

Huu ndio mkutano wa kwanza kuhudhuriwa na Sisi kama rais wa Misri baaada ya kuchaguliwa mwezi uliopita.

Jengo walilokutana viongozi wa Afrika jijini Malabo
Jengo walilokutana viongozi wa Afrika jijini Malabo Neidy Ribeiro/RFI

Mbali na maswala ya Misri, na usalama nchini Sudan Kusini na Jamhuri ya Afrika ya Kati yaliyotawala mkutano huo wa siku mbili jijini Malabo, viongozi hao pia wamezungumzia umuhimu wa kuimarisha kilimo barani Afrika ili kuzalisha chakula cha kutosha.