NIGERIA-Usalama

Nigeria : Malala Yousafzai azuru Abuja

Malala Yousafzai, akiendeleza kampeni yake ya elimu bora miongoni mwa wasichana na wanawake.
Malala Yousafzai, akiendeleza kampeni yake ya elimu bora miongoni mwa wasichana na wanawake. REUTERS/Brendan McDermid

Miezi mitatu imetimia sasa baada ya wapiganaji wa Boko Haram nchini Nigeria kuteka nyara zaidi ya wasichana mia mbili, kitendo ambacho kimewasikitisha watu wengi duniani.

Matangazo ya kibiashara

Akisheherekea mwaka wa 17 wa kuzaliwa kwake Malala Yousafzai ambaye alipigwa risasi kwenye kichwa na wanamgambo wa Taliban nchini Pakistan miaka miwili iliopita anazuru mji mkuu wa Abuja nchini Nigeria ili kuwaenzi wasichana hao na kuendeleza kampeni yake ya elimu bora miongoni mwa wasichana na wanawake.

Malala alipigwa risasi kwa kuwa alikuwa anaongoza kampeni ya wasichana kupata elimu nchini Pakistan na baada ya kupona kwake nchini Uingereza aliapa kuendelea kampeni hiyo.

Hayo yakijiri katika video iliyogunduliwa na Shirika la Habari la Ufaransa yenye dakika 16 Kiongozi wa Boko Haram Abubakar Shekau amekejeli mitandao ya kijamii na kampeni iliyoibuliwa baada ya kutekwa kwa wasichana zaidi ya mia mbili mnamo Aprili 14 katika kijiji cha kaskazini katika mji wa Chibok.

Chekau amekiri kwamba kundi la Boko Haram lilihusika katika mashambulizi yaliyotokea siku moja katika miji ya Abuja na Lagos, huku akisema kwamba kwa sasa wanaungwa mkono na makundi mengine ya kislamu: kundi la waasi wanaoshikilia jimbo la kislamu linaloundwa na maeneo kadha ya Syria na Iraq yanaoshikiliwa na waasi hao (EI), Al Qaeda na kundi la wanamgambo wa kitalibani.