CAMEROON-BOKO HARAM-Usalama

Cameroon: Paul Biya aapa kukomesha mashambulizi ya Boko Haram

Rais wa Cameroon, Paul Biya ameagiza kupelekwa kwa kikosi zaidi cha wanajeshi kaskazini mwa nchi hiyo kwa lengo la kuongeza nguvu kwa wanajeshi walioanza kukabiliana na wapiganaji wa kundi la Boko Haram la Nigeria. 

Katikati ya mji wa Yaoundé, mji mkuu wa Cameroon.
Katikati ya mji wa Yaoundé, mji mkuu wa Cameroon. Getty Images/ Tim E White
Matangazo ya kibiashara

Akizungumza mwishoni mwa juma, rais Biya amesema kuwa kutokana na kuendelea kuongezeka kwa vitendo vya uvunjifu wa amani vinavyotekelezwa na wapiganaji wa Boko Haram ambao wamevuka mpaka na kuteka raia, ameagiza kuimarishwa kwa usalama zaidi kwenye maeneo ya kaskazini mwa nchi hiyo.

Tangazo la rais Biya analitoa wakati huu ambapo jumatatu wiki hii viongozi wa mataifa 50 kutoka barani Afrika wanakutana kwa mazungumzo na rais wa Marekani Barack Obama mjini Washington ambapo ajenda kuhusu mapambano dhidi ya ugaidi inatarajiwa kujadiliwa kwenye mkutano huu.

Kwenye hotuba yake rais wa Cameroon amesifu hatua ambayo imepigwa na vikosi vyake kaskazini mwa nchi na kwamba vikosi vyake vimefanikiwa kuwafurusha wapiganaji hao na kukiri kuwa vita dhidi ya kundi hilo bado ni ngumu.

Juma lililopita rais Biya alitangaza kuwafuta kazi maofisa wake wawili wa juu wa jeshi kwenye miji ya kaskazini mwa nchi hiyo baada ya watu 15 kupoteza maisha kwenye shambulio linalodaiwa kutekelezwa na kundi la Boko haram.

Hatua hii ya Cameroon inakuja baada ya majuma kadhaa yaliyopita wanamgambo wa Boko Haram walivamia eneo la kaskazini mwa nchi hiyo ambako ndiko yamekuwa maeneo yao ya kutekeleza uhalifu na kuwateka raia kadhaa akiwemo mke wa naibu waziri mkuu.