Mkutano kati ya Afrika na Marekani waanza
Rais wa Marekani, Barack Obama, Jumatatu wiki hii anatarajiwa kuwa mwenyeji wa mkutano wa kimataifa kati yake na viongozi kutoka barani Afrika, mkutano uliolenga kuimarisha uhusiano kati ya nchi yake na bara la Afrika.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Mkutano huu unafanyika wakati huu ambapo bara la Afrika linakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo umasikini uliokithiri kwenye baadhi ya mataifa pamoja na janga la ugonjwa wa virusi vya Ebola ambao unatishia kusambaa hata kwenye mataifa ya Magharibi.
Rais Obama anatarajiwa kutumia mkutano huu kuwaeleza viongozi wa Afrika mkakati wa nchi yake katika kuimarisha biashara na nchi hizo, pamoja na namna itakavyoendelea kushirikiana na viongozi hao katika vita dhidi ya kuondoa umasikini na vitendo vya ugaidi.
Viongozi wa mataifa hamsini na Umoja wa Afrika wamealikwa. Hata hivo Jamhuri ya Afrika ya Kati, Zimbabwe, Soudani na Erythrea hazikupata mualiko. Rais wa Marekani anafanya mkutano huu ili kuanzisha uhusiano wa Marekani na bara nzima la Afrika.
Rais wa Marekani, ambaye baba yake ni raia wa Kenya, hajatekeleza kile ambacho raia wa bara la Afrika walikua wanasubiri kutoka kwake.
Wachambuzi wa masuala ya siasa wamesema mkutano huo ni kipimo kwa utawala wa Barack Obama hasa kwa kuboresha uhusiano kati ya Marekani na bara la Afrika.