MAREKANI-AFRIKA-Ushirikiano-Biashara

Marekani yakubali kuwekeza zaidi ya dola bilioni 30 barani Afrika

WASHINGTON, Agosti 6, 2014 (AFP) - Rais Barack Obama ametangaza Jumanne wiki hii uwekezaji wa zaidi ya dola bilioni 30 wa nchi yake barani Afrika. Obama amesema sekta ya umma na sekta binafsi ndizo zinazolengwa kwa uwekezaji huo, huku akitoa wito kwa viongozi wa Afrika kuboresha mazingira ya kisiasa na kiuchumi yanayoendana na biashara.

Viongozi wa mataifa ya kiafrika wakiandaliwa hafla na ikulu ya Washington.
Viongozi wa mataifa ya kiafrika wakiandaliwa hafla na ikulu ya Washington. REUTERS/Larry Downing
Matangazo ya kibiashara

"Marekani inawekeza kwa kiasi kikubwa katika muda mrefu, katika maendeleo barani Afrika," Obama amesema jumanne wiki hii kwa siku ya pili ya mkutano huo wa kilele unaojumuisha viongozi zaidi ya 40 kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika.

 Washington, imeanzisha mikakati yake ya kushindana na mataifa ya Ulaya na China kwa kuwekeza barani Afrika, baada ya kuonekana kutotekeleza ahadi alizozitoa Barack Obama alipochukua madaraka mwaka 2009. Obama ameelezea kwamba ushirikiano wa kibiashara na bara zima la Afrika ni sawa na ule uliyotekelezwa kwa taifa la Brazil peke yake. "Kati ya bidhaa zote zinazotoka nchini Marekani na kuuzwa duniani kote, asilimia 1 tu inaingia kusini mwa jangwa la Sahara," ameongeza Obama.

 Rais wa Marekani ametangaza kuwa makampuni ya Marekani - Marriott, Coca-Cola na General Electric walikuwa na nia kwa muda mrefu ya kuwekeza dola bilioni 14 barani Afrika, hasa katika sekta za nishati, maji, hoteli, ujenzi, benki aidha katika sekta ya teknolojia ya habari .

Sekta binafsi pia imeongeza ahadi zake za uwekezaji katika mpango uliyoitwa “ Power Africa mpango, ambao una lengo la kuzidisha mara mbili huduma ya umeme kusini mwa jangwa la Sahara. Kwa jumla, ikijumlishwa na mchango wa Benki ya Dunia na serikali ya Sweden, dola bilioni 26 zinatazamiwa kuwekezwa katika mradi huu.

Barack Obama atazamia kuzungumzia jumatano wiki hii na viongozi wa mataifa ya Afrika kuhusu usalama.