UN-SUDANI KUSINI-Vikwazo-Siasa

Sudani Kusini: UN yaonya pande zinazozozana

Rais wa Sudani Kusini, Salva Kiir (kushoto) na kiongozi wa waasi, Riek Machar (kulia) wakimaliza swala kabla ya kutia saini kwenye mkataba wa kusitisha machafuko, mjini Addis Ababa.
Rais wa Sudani Kusini, Salva Kiir (kushoto) na kiongozi wa waasi, Riek Machar (kulia) wakimaliza swala kabla ya kutia saini kwenye mkataba wa kusitisha machafuko, mjini Addis Ababa. EUTERS/Goran Tomasevic (

Ujumbe wa baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa umewaonya viongozi wanaopingana nchini Sudan kusini leo jumatano kuwa watakabiliwa na vikwazo iwapo vita vya wenyewe kwa wenyewe vinavyolisukuma taifa hilo changa katika ukingo wa janga la njaa havitakoma.

Matangazo ya kibiashara

Misimamo ya makundi mawili yanayohusika katika mgogoro unaoendelea nchini Sudani Kusini tangu mwezi Desemba, inaonesha kufifia kwa matumaini ya amani, amesema balozi wa Uingereza kwenye Umoja wa Mataifa, Mark Lyall Grant, akiwa ziarani Juba.

“Tumekutana kwa mazungumzo na rais wa Sudani Kusini, Salva Kiir, na makamu wake wa zamani, Riek Machar, hakuna hata mmoja aliyetuthibitishia mchango wake kwa jitihada za mchakato wakumaliza mzozo unaoendelea aidha kuhusu mkataba wa haraka wa kusitisha machafuko katika mazungumzo yanayoendelea mjini Addis Abeba, nchini Ethiopia.

Kwa upande wake balozi wa Marekani katika  Umoja  wa  Mataifa Samantha Power  amesema  baada ya kukutana  na rais Salva  Kiir kuwa baraza  hilo  limeweka  wazi kwamba  liko  tayari kuweka  vikwazo iwapo kutakuwa  na  watu wanaochafua mchakato  wa  amani , ama kuendelea na ukiukaji wa haki  za  binadamu.

Wawakilishi wa baraza hilo lenye wajumbe 15 , ambao wamewasili katika  mji  mkuu  wa Juba jumatano wiki hii katika ziara ya  siku  mbili, wanatarajiwa  kukutana  na kiongozi wa waasi Riek Machar.

Maelfu  ya  watu  wameuwawa  na zaidi  ya  watu  milioni 1.5 wamekimbia  makaazi yao kutokana na mapigano yaliyochukua zaidi  ya  miezi  minane  yaliyozushwa  na mvutano wa kutaka  madaraka kati  ya  rais Salva Kiir  na naibu  wake  aliyemfuta  kazi Riek Machar.