SOMALIA-AL SHABAB-Ugaidi-Usalama-Haki za binadamu

Somalia: watoto wanaozuiliwa katika magereza wanakabiliwa na vitendo vya udhalilishaji

Leila Zerrougui, mkuu wa tume ya Umoja wa Mataifa inayohusika na watoto.
Leila Zerrougui, mkuu wa tume ya Umoja wa Mataifa inayohusika na watoto. AFP/MOHAMMED HUWAIS

Wanajeshi watoto waliokuwa wanatumikishwa kwa nguvu nchini Somalia na ambao wanashikiliwa kwenye magereza maalumu yanayofadhiliwa na mataifa ya kigeni, wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya udhalilishaji na mateso badala ya kurekebishwa tabia, amesema mkuu wa tume ya Umoja wa Mataifa inayohusika na watoto.

Matangazo ya kibiashara

Leila Zerrougui, mjumbe maalumu wa UN anayehusika na watoto kwenye maeneo ya migogoro, amesema watoto hao ambao wanahifadhiwa kwenye jela maalumu zilizokuwa zitumike kuwarekebisha, wamekuwa wakinyanyaswa na kuendelea kushikiliwa bila kufunguliwa mashtaka.

Leila ametolea mfano kituo cha Serendi kilichoko mjini Mogadishu ambacho kinafadhiliwa na serikali ya Norway, kinawahifadhi zaidi ya watoto 55 waliokuwa wanapigana sambamba na kundi la Al-Shabab lakini wamekuwa wakinyanyaswa.

Mjumbe huyo ametaka nchi zinazofadhili jela hizo kufanya uchunguzi na kuwachukulia hatua maofisa wa Somalia wanahusika na vitendo hivyo.

“watoto hao wanazuiliwa bila kuheshimu utaratibu wowote”, amesema Leila Zerrougui, mkuu wa tume ya Umoja wa Mataifa inayohusika na watoto.

Afisa huyo amekemea vikali gereza la Serendi mjini Mogadiscio, ambalo linadhaminiwa na serikali ya Norway, ambapo watoto 55 wanazuiliwa.