DRC-Ebola-Afya

DRC: Watu wawili waambukizwa ugonjwa wa Ebola

Ugonjwa wa Ebola umeanza kushuhudiwa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia. Waziri wa afya, Felix Kabange Numbi, ametangaza kwamba watu wawili wameambukizwa Homa ya Ebola katika mkoa wa Equateur kwa jumla ya wagonjwa 11 waliyotengwa mbali na watu kwa kuhofia maambukizi.

Virusi vya Ebola.
Virusi vya Ebola. REUTERS/Frederick Murphy
Matangazo ya kibiashara

Kwa mujibu wa viongozi , virusi hivyohuenda havikutokea katika nchi jirani.
“Ni vigumu kufika au kutembelea eneo kunakoshuhudiwa ugonjwa huo, na ndio maana nasema kwamba ugonjwa huo haukutokea nchi jirani”, amesema Numbi.

Inasadikiwa kuwa ugonjwa huo uliletwa na mwanamke mmoja, aliefariki Agosti 11, baada ya mume wake kuwinda nyani. Kabla ya kufariki, mwanamke huyo alimuambukiza daktari aliye kuwa akimfuatilia kimatibabu, na baadaye alimuambukiza mume wake. Vipimo vilionesha kuwa watu hao walifariki kutokana na ugonjwa wa Ebola. Hayo yamethibitishwa na waziri wa afya Felix Kabange Numbi. Ebola inatokea kwenye msitu wa Equateur, katika kijiji cha Djera (kilomita 300 mashariki mwa Mbandaka), maabara ya mjini Kinshasa yamethibitisha.

Wizara ya afya imechukua hatua za haraka ili kudhibiti ugonjwa huo, hususan kutenga eneo kunakoripotiwa ugonjwa wa Ebola kwenye umbali wa kilomita mraba 100, huku kati ya watu 30,000 na 40,000 wazuiliwa kutoondoka katika eneo hilo. Askari polisi wamewekwa karibu na eneo hilo ili kuzuia watu kuingia maeneo mengine jirani. Shirika la madaktari wasio na mipaka (MSF), linapania kutuma haraka iwezekanavyo wafanyakazi wake katika eneo la Djera.

Wizara ya afya imebaini kwamba Homa ya Ebola haijashuhudiwa katika mji wa Kinshasa na kwenye makao makuu ya mkoa wa Equateur, Mbandaka. Ni kwa mara ya saba Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inashuhudia ugonjwa wa Ebola tangu miaka 30 iliyopita.