RWANDA-FDLR-Usalama, Siasa

Maiti kwenye ziwa Rweru: Upinzani nchini Rwanda unaomba ufanyike uchunguzi

Frank Habineza, kiongozi wa chama cha kijani nchini Rwanda.
Frank Habineza, kiongozi wa chama cha kijani nchini Rwanda. Rwandagreendemocrats.org

Kauli za kulani mauaji na kuomba uchunguzi ufanyike zimeanza kutolewa nchini Rwanda baada ya kuonekana miili ya watu waliouawa kwenye ziwa Rweru kwenye mpaka wa Burundi.

Matangazo ya kibiashara

Upinzani nchini Rwanda umeomba uchunguzi ufanyike, wakati ambapo serikali ya Kigali ilibaini hivi karibuni kwamba miili ya watu hao walioonekana kwenye ziwa Rweru (Burundi), si raia wa Rwanda.

Serikali hiyo imesema miili ya watu watano ndio ilioonekana kwenye ziwa Rweru, huku wavuvi wanaoendesha shughuli zao kwenye ziwa hilo wakibaini kwamba wameona miili ya watu zaidi ya arobaini zikiwa kwenye maji ya ziwa Rweru.

Viongozi wa Rwanda hata viongozi wa Burundi, kila upande umebaini kwamba miili hiyo ya watu waliotupwa kwenye ziwa Rweru si raia kutoka mataifa hayo mawili.

Habari hii ya kuonekana kwa maiti kwenye ziwa Rweru imezua hisia tofauti upande wa upinzani nchini Rwanda ikiwa ndani na nje ya nchi. Upinzani nchini Rwanda umeomba kufanyike uchunguzi wa kina wa vipimo vya damu ili kubainika uraia wa watu hao.

Hata hivi shirika la kimataifa la haki za binadamu la Human Right Watch hata serikali ya Marekani vilibaini hivi karibuni kwamba zaidi ya watu kumi walikamatwa nchini Rwanda na hawajulikani waliko.

Kiongozi wa chama cha kijani, Frank Habineza, ameelezea wasiwasi wake kutokana na hali hiyo. Mmoja kati ya wajumbe wa chama hicho alipotezwa mwishoni mwa mwezi juni.
“Tunaomba kufanyike uchunguzi wa kina wa vipimo vya damu na vidole ili kubainisha iwapo raia hao ni kutoka Rwanda au la”, amesema Habineza.

Kwa upande wake Boniface Twagirimana, wa tawi la chama cha FDU kinachoongozwa na Victoire Ingabire, ambaye anaishi Kigali, amekua akijiuliza ni katika mazingira gani watu hao waliuawa, na baadae kutupwa kwenye ziwa.

Vyama sita vya upinzani viliyoko nje ya nchi PDP, PDR PS Imberakuri, RNC, Amahoro People's Congress na tawi lingine la FDU wametoa tangazo la pamoja wakiomba uchunguzi wa kina ufanyike.