DRC-Uteuzi-Usalama-Siasa

DRC: Jenerali Emmanuel Lombe mkuu wa majeshi Kivu Kaskazini

Gwaride la wanajeshi katika mji wa Goma wakisheherekea miaka 54 ya uhuru, Juni 30 mwaka 2014.
Gwaride la wanajeshi katika mji wa Goma wakisheherekea miaka 54 ya uhuru, Juni 30 mwaka 2014.

Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo FARDC limemteuwa kamanda mpya kuchukua nafasi ya General Lucien Bahuma Ambamba aliyefariki mwishoni mwa juma lililopita Afrika Kusini.

Matangazo ya kibiashara

Brigedia Jenerali Emmanuel Lombe, ndiye kamanda mpya wa mkoa wa nane wa kijeshi 8 jimboni Kivu Kaskazini ambapo mara baada ya kuteuliwa amewasili na kuanza kazi jumanne wiki kwa kukutana na maafisa wa jeshi la FARDC na askari wa kulinda amani MONUSCO mjini Goma.

Jenerali Lombe amepewa pia jukumu la kuliongoza jeshi jimboni humo katika Operesheni maarufu kwa jina la 'Sokola' dhidi ya waasi wa Uganda wa ADF-Nalu mjini Beni ambapo operesheni hiyo inatarajiwa kuendelea kwa msaada wa MONUSCO.

Hata hivyo, Kiongozi huyo mpya atakabiliana na tatizo la makundi yenye kumiliki silaha katika maeneo mengine ya mkoa wa Kivu Kaskazini ikiwemo Walikale, Masisi, Rutshuru, Lubero na Beni, ambapo makundi haya bado hayajaridhia mchakato wa kuwasambaratisha, kuwapokonya silaha, na kuwaunganisha na jamii zao kulingana na mpango wa DDRR wa serikali ya Kinsasha.

Jenerali Lombe alipata mafunzo ya kijeshi katika chuo cha EFO Kananga mkoani Kasai Occidental na kuongoza operesheni maarufu kwa jina la 'Rudiya 2', dhidi ya waasi wa Uganda wa LRA eneo la Dungu, jimbo la Province Orientale mwaka 2011 hadi 2013 na baadaye kupewa majukumu mengine kwenye makao makuu ya jeshi la FARDC mjini Kinshasa hadi uteuzi wake mpya.

Hayo yakijiri watu 31 wanaripotiwa kufariki tangu kuzuka kwa Homa ya Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambapo tayari watu sitini wanasadikiwa kuambukizwa ugonjwa huo.

Pamoja na takwimu hizo, waziri wa Afya nchini humo Felix Kabange Numbi amesema kuwa bado yapo matumanini kuudhibiti ugonjwa huo baada ya kuiweka wilaya ya Boende karantini na ambapo jumatano wiki hii anatarajiwa kuzuru eneo hilo kwa tathmini zaidi.