SIERRA LEONE-MAREKANI-IMF-Ebola-Afya

IMF mbioni kukabiliana na kuenea kwa virusi vya Ebola

Wakaazi wa mji wa Freetown waendelea kufanyiwa vipimo vya damu ili kukabiliana na kuenea kwa virusi vya Ebola, Septemba 19 mwaka 2014.
Wakaazi wa mji wa Freetown waendelea kufanyiwa vipimo vya damu ili kukabiliana na kuenea kwa virusi vya Ebola, Septemba 19 mwaka 2014. Reuters/Bindra/UNICEF

Rais wa Sierra Leone, Ernest Bai Koroma ambaye nchi yake imeathirika kwa sehemu kubwa na ugonjwa wa Ebola, amesema kuwa harakati za dunia kukabiliana na virusi hivi ziko taratibu mno ukilinganisha na kasi ya kuenea kwa ugonjwa huu.

Matangazo ya kibiashara

Rais Koroma ameyasema haya wakati wa mkutano wa kimataifa wa shirika la fedha duniani IMF na Benki ya dunia, ambapo akaonya kuhusu kuendelea kwa hali ya taratibu ya kukabiliana na ugonjwa huu ambao kasi yake ni kubwa zaidi ya juhudi zinazofanyika.

Kauli ya rais Koroma iliungwa mkono na rais wa Benki ya Dunia, Jim Yong Kim ambaye amesema kuwa kwa sasa ni lazima dunia iungane na kuongeza kasi ya kukabiliana na ugonjwa huu ama sivyo bara zima la Afrika liko kwenye hatari ya kukumbwa na ugonjwa huu.

Katika hatua ya kushangaza, kwa mara ya kwanza mkurugenzi wa shirika la fedha duniani IMF, Christine Lagarde, amesema kuwa shirika lake linalazimika kuachana na sera ya awali ya kutofadhili miradi ya afya na badala yake litatoa fedha kusaidia kukabiliana na kuenea kwa virusi vya Ebola.

Wataalamu wa Afya wa Marekani wameonya kuhusu kuendelea kuenea kwa kasi kwa virusi vya Ebola na kudai kuwa iwapo havitadhibitiwa mapema huenda vikawa janga kubwa zaidi kuliko hata lile la maradhi ya virusi vinavyoambukiza ugonjwa wa Ukimwi.