BURKINA FASO-COMPAORE

Rais Compaore atangaza kujiuzulu

Rais wa Burkina Faso, Blaise Compaore ambaye siku ya Ijumaa ametangaza kujiuzulu
Rais wa Burkina Faso, Blaise Compaore ambaye siku ya Ijumaa ametangaza kujiuzulu RFI

Rais wa Burkina Faso, Blaise Compaore muda mfupi uliopita ametangaza kujiuzulu nafasi yake kupitia tangazo lililotelewa na jeshi ambalo limesema kwa sasa ndilo linalodhibiti usalama nchini humo. 

Matangazo ya kibiashara

Uamuzi wa rais Compaore unakuja ikiwa zimepita saa chache toka atangaze kutokuwa tayari kujiuzulu nafasi hiyo licha ya shinikizo na maandamano ya wananchi ambao wanapinga kiongozi huyo kujiongezea muda wa kukaa madarakani.

Kanali Boureima Farta ambaye ametangaza jeshi kuchukua mamlaka, amesema kuwa kwasasa rais Blaise Compaore na familia yake wameondoka katika mji mkuu wa nchi hiyo Ouagadougou.

Rais wa Ufaransa, Francois Hollande amepongeza uamuzi wa rais Compaore ambapo mapema aliamini kuwa kiongozi huyo angeondoka madarakani kwa hiari.

Jumuiya ya kimataifa inataka kuwepo kwa hali ya utulivu wakati huu jeshi likichukua nchi.

Kwa mujibu wa katiba ya Burkina Faso uchaguzi mkuu unapaswa kufanyika ndani ya siku 90 toka rais alipojiuzulu ambapo sasa jeshi linatakiwa kutangaza mtu ambaye ataongoza nchi hiyo kwa kipindi cha siku tisini.

Umoja wa Ulaya EU umewataka wananchi wa Burkina Faso kuwa waamuzi wa hatma ya nchi yao baada ya rais Blaise Compaore kutangaza kujiuzulu nafasi yake na jeshi kuchukua hatamu ya muda.

Katika taarifa iliyotolewa na umoja huo wa nchi 28 za Ulaya, imesema kuwa wako tayari kusaidia kufanyika kwa uchaguzi huru na wa haki nchini humo kama alivyopendekeza rais Blaise Compaore kwenye barua yake wakati akitangaza uamuzi wa kujiuzulu.

Tangazo la kujiuzulu kwa rais Compaore lilipokelewa kwa shamrashamra na waandamanaji waliokuwa nje ya makao makuu ya jeshi mjini Ouagadougou ambapo lilitangaza kuwa Compaore si rais tena wa nchi hiyo.