MALI-ULINZI-MUJAO-ANSAR DINE-AQMI

Watu 8 wauawa katika shambulizi dhidi ya kambi

Kwa uchache watu wanane wameuawa Jumatatu Januari 5 katika kijiji cha Nampala, kusini mwa mji wa Tombouctou nchini Mali, karibu na mpaka wa Mauritania.

Matangazo ya kibiashara

Shambulio hili limekua limelenga ngome ya askari wa Mali. Hakuna kundi ambalo limedai kuhusika na shambulio hilo, lakini vyanzo kadhaa vilivyowasiliana na RFI, vimebaini kwamba shambulio hilo limeendeshwa na " makundi ya kigaidi".

Makundi ya Mujao, Ansar Dine na Aqmi yamekua yakiendesha mashambulizi ya mara kwa mara nchini Mali.

Hata hivyo hakuna kundi miongoni mwa makundi hayo ambalo limedai kuhusika katika shambulio hilo, lakini mpaka sasa vyanzo viliyowasiliana na RFI bado vinaendelea kubaini kwamba shambulio hilo limetekelezwa na “ makundi ya kigaidi”.

Watu hao wenye silaha waliingia Jumatatu Januari 5 mchana katika kijiji cha Nampala kusini mwa mji wa Tombouctou. Walipowasili eneo la Mashariki mwa kijiji hicho, waliegesha magari yao na kutembea kwa mguu hadi Kusini Mashariki mwa mji wa Tombouctou na kuanza kushambulia kambi ya kijeshi ambamo alikua akiishi mkuu wa mji huo.

Watu hao wenye silaha waliondoka katika kijiji hicho baada ya ndege za kijeshi za kikosi cha wanajeshi wa Ufaransa (Barkhane) kupaa katika anga ya kijiji cha Nampala, na kutishia kuingilia kati.

Mashambulizi hayo yamegharimu maisha ya watu wanane ambao walikua wamevaa sare ya jeshi, na wengine wengi kujeruhiwa. Hali ya utulivu imeanza kurejea tangu jana Jumatatu jioni.