Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo

UN yaingoja saini ya rais Kabila kushambulia kundi la FDLR

askari wa kikosi cha kulinda amani nchini DRC MONUSCO,wakiwa katika operesheni zao
askari wa kikosi cha kulinda amani nchini DRC MONUSCO,wakiwa katika operesheni zao MONUSCO/Force

Umoja wa Mataifa bado unasubiri saini ya Rais Joseph Kabila katika mpango wa jeshi la pamoja la kuwafukuza waasi kutoka mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Umoja wa Mataifa umesema jana Ijumaa.

Matangazo ya kibiashara

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amewaambia waandishi wa habari kwamba rais Kabila bado hajasaini azimio la pamoja kuhusu operesheni ya kijeshi licha ya kuombwa kufanya hivyo na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Katibu Mkuu wa Umoja huo Ban Ki-moon zaidi ya wiki moja iliyopita.

Kikosi cha Umoja wa Mataifa nchini DRC MONUSCO chenye askari elfu ishirini kinajiandaa kuzindua mashambulizi dhidi ya waasi wa Kihutu, lakini mafanikio ya kikosi hicho yanategemea kwa kiasi kikubwa ushiriki wa majeshi ya serikali ya Kongo.

Waasi kutoka kundi la FDLR wanakabiliwa na hatua ya kijeshi baada ya kushindwa kufikia makataa ya Januari 2 tarehe ya mwisho iliyowekwa na viongozi wa Afrika na Umoja wa Mataifa kwa ajili yao kujisalimisha.

Umoja wa Mataifa unashinikiza kunyang'anywa silaha kwa waasi kadhaa na makundi ya waasi baada ya miongo miwili ya vita mashariki mwa DR Congo, ambayo kwa kiasi kikubwa imechochewa na biashara ya faida kubwa katika madini.