DRC-FDLR-MONUSCO-USALAMA

Operesheni ya kuwasaka waasi wa FDLR yaanza

Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo limeanza operesheni ya kuwapokonya silaha wapiganaji wa Kihutu wa Rwanda wa FDLR, mashariki mwa DRC.
Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo limeanza operesheni ya kuwapokonya silaha wapiganaji wa Kihutu wa Rwanda wa FDLR, mashariki mwa DRC.

Vikosi vya Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya congo vimeanzisha Alhamisi Januari 29 operesheni ya kijeshi "Sokola2" kwa lengo la kuwapokonya silaha waasi wa Kihutu wa Rwanda wa FDLR.

Matangazo ya kibiashara

Mkuu wa majeshi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, jenerali Didier Etumba amethibitisha taarifa hio katika mkutano na waandishi wa habari mjini Beni katika mkoa wa Kivu Kaskazini, akiwa pamoja na mkuu wa majeshi ya Umoja wa Mataifa nchini Congo, Monusco.

" Kwa hio leo tumeanzisha operesheni mpya ya kijeshi dhidi ya wapiganaji wa FDLR ili kuwashawishi wajisalimishe na warejesha silaha. Tumepokea kwa mara nyingine tena msaada wa Monusco kwa ajili ya shughuli hizo", amesema mkuu wa majeshi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Didier Etumba.

Mkuu wa majeshi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Didier Etumba (katikati),katika mkutano na waandishi wa habari mjini Goma, Aprili 11 mwaka 2012.
Mkuu wa majeshi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Didier Etumba (katikati),katika mkutano na waandishi wa habari mjini Goma, Aprili 11 mwaka 2012. AFP/ PHIL MOORE

Kwa mujibu wa jenerali Didier Etumba, waasi wa Rwanda wa FDLR wanakadiriwa kufikia wapiganaji zaidi ya elfu ambao watapokonywa silaha na jeshi la Congo, FARDC, kwa msaada wa Monusco.

Hii ni hatua iliyosubiriwa kwa muda tangu makataa ya mwisho kutolewa mnamo Januari 2 mwaka 2015 na jumuiya ya kimataifa kwa waasi kusalimu amri na kurejesha silaha au mashambulio makali dhidi yake yaanzishwe.

Maafisa wa Umoja wa Mataifa walioko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, wamesema kuwa operesheni hiyo bado haijaanza.

Kwa mjibu wa jenerali Dos Santos Cruz, mianya yote ya kutorokea waasi hao imezibwa na wanajeshi wa Congo huku vikosi vya Umoja wa Mataifa wakitoa usaidizi wa silaha na vifaa vinginevyo.

Waasi wa Kihutu wa Rwanda wa FDLR, kilomita 150 kaskazini mashariki mwa Goma, mwaka 2009.
Waasi wa Kihutu wa Rwanda wa FDLR, kilomita 150 kaskazini mashariki mwa Goma, mwaka 2009. AFP/ Lionel Healing

FDLR imesema kuwa haitajitetea katika vita hivyo, lakini inataka kuzungumza na serikali ya Rwanda, inayoilaumu kwa kuhusika katika mauaji ya kimbari yaliyotokea Rwanda mwaka 1994.